Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KAIMU Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Dkt. Gervas Kasiga amewataka wasanii kutunza vipaji vyao kwa kuwa ndio vinavyowapatia fursa ya vipato.
Dkt. Kasiga amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Washirika wa Tamasha na Tuzo za Filamu Tanzania 2025.
Katika uzinduzi huo amesisitiza kuwa vipaji ndio sehemu kubwa ya kutoa ajira hapa nchini hivyo wasanii wavitunze.
Kwa maelezo yake tamasha hilo linaratibiwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bodi ya Filamu Tanzania pamoja na Studio 19 Limited.
Amesema tamasha hilo la nne toka kuanzishwa kwa matamasha kama hayo linapozinduliwa ubora wake utakuwa umeongezeka tofauti na matamasha mengine yaliyopita.
Amesema lengo la tamasha hilo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuanzisha na kuratibu program za kufufua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafila.
Amesema Rais Samia ameonesha ana mapenzi na tasnia ya filamu kwa kuwa hata yeye alishiriki katika kutengeneza filamu.
Akielezea mafanikio ya tamasha hilo amesema ni kutambua na kufufua vipaji mbalimbali vilivyojificha na kutolea mfano kama uandishi bora wa miswada, wapiga picha bora na mambo mengineyo.
Pia amesema tamasha limekuza hamasa kwa wadau wa filamu kuzalisha kazi bora zinazokidhi vigezo ndani na nje ya nchi.
Pamoja na kuwa na mchango katika kukuza ushirikiano na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Filamu 19, Sama Jahanpour amesema nguvu iliyokuwak wenye sanaa ya filamu ni nyenzo muhimu katika kueneza sanaa za masimulizi.
Pia amesema picha jongefu ina nguvu ya kufikia watu wengi, vile vile ina nguvu kubwa ya kuhamasisha watu.
Mkurugenzi mwingine wa Studio 19 Limited, Brian Paul amesema uzinduzi huo utawaweka wadau kutoka sekta mbalimbali za ubunifu pamoja ili kuorodhesha mustakabali wa tasnia hiyo.
“Tamasha la Filamu na Tuzo za Tanzania 2025 ni mpango kabambe unaolenga kuiweka Tanzania kama kitovu cha ubunifu wa kimataifa, kwa kutumia uwezo wa filamu kukuza utamaduni, kusukuma ukuaji wa tasnia na uvumbuzi wa nishati.
‘Uzinduzi huu ni hatua muhimu katika safari hii, iliyoundwa ili kukuza mazungumzo, kuhamasisha ushirikiano, na kuoanisha malengo ya pamoja ya tamasha,” amesema..
Amefafanua kuwa tamasha hilo dhamira yake ni kutumia uwezo wa kusimulia hadithi kwa ajili ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Amesema tamasha hilo litafichua vipaji ambavyo havijatumiwa katika tasnia ya ubunifu, kuunganisha Washika dau mbalimbali na kukuza uwezo wa sekta hiyo kuleta mabadiliko yenye matokeo.