Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema serikali inahimiza matumizi ya vyombo vya mashauriano ili kuzungumza na kufikia mahali pazuri kwenye masuala yahusuyo wafanyakazi.
Ridhiwani amesema hayo alipokuwa akizindua Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), jijini Dodoma.
Akizungumzia vyombo hivyo amevitaja kuwa ni Bodi ya Ushauri wa Masuala ya Kazi, Uchumi na Kijamii (LESCO), Bodi ya Mishahara pamoja na Mabaraza ya Wafanyakazi ili kuweza kuzungumzia masuala ya wafanyakazi na kufikia muafaka.
Pia Waziri Ridhiwani amesema mabadiliko ya sheria mbalimbali yanaendelea ikiwemo suala la Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kwamba ni moja kati ya sheria zilizoguswa.
“Timu ya wataalamu ipo Morogoro ikifanya mapitio mbalimbali ya sheria na kanuni zinazohusu vyama vya wafanyakazi. Itakapokuwa tayari tunakuja kuwashirikisha tukitambua ninyi ni wadau muhimu.
“Mabadiliko ya sheria tunayotaka kuyafanya na mapitio ya kanuni tunayoendelea kuyafanya nina imani kwa namna moja au nyingine yanagusa maslahi ya wafanyakazi.
“Na ninyi kama chama kinachosimamia maslahi hayo ni muhimu kushirikishwa na ili sheria iweze kuwa na tafsiri ambayo inakusudiwa,” amesema.
Awali Katibu Mkuu TUCTA, Hery Mkunda alimweleza Waziri Ridhiwani kwamba, mwaka 2018/19 Sheria ya Utumishi wa Umma rejeo la 2019 ilifanyiwa marekebisho yanayomnyima mtumishi wa umma haki ya kutumia mfumo wa CMA na mahakama katika kutatua mgogoro wa kikazi.
Amesema mabadiliko hayo yamesababisha athari kubwa kwa watumishi wa umma. Hivyo TUCTA inapendekeza milango ya majadiliano ifunguliwe ili yafanyike marejeo ya sheria hiyo lengo likiwa mtumishi wa umma kurejeshewa haki yake ya kuamua mfumo atakaoona unafaa kutatua mgogoro wake, jambo ambalo Waziri Ridhiwani tayari amelitolea ufafanuz