Na Lucy Ngowi
TAKWIMU zinaonyesha uhitaji wa mbegu bora za viazi vitamu kwa Kanda ya Ziwa ni vipando milioni 23, ilhali idadi iliyotumiwa na wakulima ilikuwa ni vipando chini ya milioni tano tu.
Mkuu wa Programu ya Utafiti wa zao hilo la viazi vitamu, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Kituo cha Ukirigulu Mwanza, Dkt. Hadija Ally ameelezea takwimu hizo za mwaka 2022/ 2023.
Dkt. Hadija ameeleza hayo katika ufunguzi wa mafunzo kwa watafiti wa viazi na muhogo yanayofanyika kwa siku nne Mkoani Mwanza katika Kituo cha TARI Ukiriguru.
Akielezea athari za ugonjwa wa virusi vya viazi vitamu, Dkt. Hadija amesema mkulima hawezi kupata mavuno ya aina yoyote endapo shamba lake limeathiriwa kwa asilima 100 na virusi.
Amesema ujio wa teknolojia ya kutambua na kuzalisha mbegu stahimilivu dhidi ya virusi utaleta tija katika kilimo cha viazi vitamu.
Amesema viazi vitamu ni miongoni mwa mazao ya chakula yanayotegemewa katika maeneo mengi nchini, hivyo uzalishaji utakapoongezeka utasaidia kuimarisha usalama wa chakula.
Naye Mtafiti wa mihongo kituo cha TARI Ukiriguru, Salum Kasele amesema uzalishaji wa muhongo nchini ni tani 8.6 badala ya tani 30 kwa hekta ambazo ndizo kiwango cha uzalishaji wenye tija.
Amesema wastani wa muda wa kuanza kutafiti mbegu hadi kuisajili kwa kutumia njia ya kawaida inaenda hadi miaka 10, hivyo kupitia mafunzo hayo muda wa kuzalisha mbegu hadi kumfikia mkulima unategemewa kufikia wastani wa miaka mitano.
Mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa TARI na Taasisi nyingine, ikiwemo Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha kitropiki (IITA), Shirika la Kimataifa la Utafiti (CIAT) na Maabara ya uchunguzi wa virusi ya Ujerumani (DSMZ).
Ushirikiano unalenga kujengeana uwezo wa teknolojia za uzalishaji wa haraka wa mbegu za mazao ya mizizi zisizokuwa na magonjwa ili kuwafikia wakulima kwa wakati na hivyo kuchangia kuongezeka tija.