Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: SERIKALI inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati. wa Anga za Juu utakaoiwezesha Tanzania kurusha satelaiti.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mpango mkakati huo ni wa miaka mitano kuanzia 2024/25 hadi 2029/30.
Majaliwa amesema hayo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Kongamano la Nane la Mwaka la TEHAMA, lililofanyika Dar es Salaam.

Amesema Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ( DIT), imepata mradi wa Utafiti wa kuwezesha urushaji wa satelaiti unaosimamiwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya anga za juu ikishirikiana na Taasisi ya Anga za Juu ya Japan (JAXA).
“Katika eneo hili Maandalizi ya utungwaji wa Sera, Sheria na uridhiwaji wa mikataba ya Kimataifa ya masuala ya anga za juu yanaendelea,” amesema.
Majaliwa ameitaka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iwakusanye vijana wabunifu wenye uwezo wa kubuni teknolojia zenye manufaa kwa Taifa.
“Lakini simamieni hizi tafiti zenye kutoa matokeo na vijana hao waendelee kupewa fursa na kazi hizo ziingie kwa jamii na zianze kutumika,” amesema.
Kwa Upande wake Waziri Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ambapo kwa mwaka fedha 2023/24 jumla ya urefu wa kilomita 1,592 za mkongo wa taifa zimejengwa na kufika katika wilaya 83.
“Pia umoja wa watoa huduma za mawasiliano wameweza kujenga jumla ya kilomita 2,595 ambazo zinafanya mkongo wa taifa kuwa na kilomita 13,820.
“Wizara imehamisha shughuli zote zinazohusiana na ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano na kituo cha kuhifadhia data (NIDC) kwenda katika Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),” amesema.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrka, Nardos Bekele-Thomas amempongeza Rais Samia kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha Tanzania inatumia ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika kuchagiza Maendeleo Endelevu nchini.