– Awataka watumishi wa Umma Kuwatembelea Wananchi Walipo
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Maofisa masuhuli kwenye Halmashauri nchini kuweka msisitizo wa kutumia mifumo ya kielektroniki katika makusanyo badala la kukusanya kwa fedha taslimu.
Majaliwa amesema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza mapato katika maeneo yao na kuepuka vishawishi vya kutumia vibaya fedha za umma ambazo zinakusanywa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema hayo leo Oktoba 05, 2024 alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam.
“Suala la mapato ni lazima mliwekee msisitizo ili tupate matokeo mazuri kwenye halmashauri zetu,” amesema.
Pia ametoa wito kwa wakurugenzi wa Halmashauri kutumia mapato ya ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali kuu pekee.
“Acheni kutegemea mapato ya Serikali kuu pekee, tunataka kuona mapato ya ndani yanatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo.,” amesema.

Amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu ili mipango na malengo ya Serikali ya kuwahudumia Watanzania yaweze kutimia.
Majaliwa amesema watumishi wa umma ni wahudumu wa wananchi hivyo wanapaswa kuwahudumia ipasavyo kwenye maeneo yao na kutatua kero zao.
“Sisi tunataka tuone mkifanya kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu usipofanya hivyo utakuwa unakosa sifa za kuwa mtumishi wa umma.
“Sisi ni watumishi wa umma na ni wahudumu wa Wananchi, tumefunga mikataba ili tuwe wahudumu wao, tumekubali hilo, twende tukafanye kazi, tunapaswa kuwatembelea walipo, kila mmoja ana wajibu wa kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yao,” amesema.