Na Mwandishi Wetu’
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA),umetoa sh. Milioni 38.2 kwa ajili ya kufungwa mfumo wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia Suluhu Hassan mkoani Ruvuma.
Shule hiyo ya kisasa yenye wanafunzi zaidi ya 540 iliyopo Wilaya ya Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma imezinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 27, Mwaka huu.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti REA, Godfrey Chibulunje ameshukuru serikali kwa kutoa fedha zinazowezesha wakala kutekeleza miradi yake mbalimbali kwa wakati ikiwamo miradi ya nishati safi ya kupikia.
Chibulunje amesema, REA itahakikisha shule mbalimbali zinafungwa mfumo wa nishati safi wa kupikia na kuachana na matumizi ya kuni.
Amesisitiza kuwa wakala huo umesaini mikataba ya zaidi ya Sh. Bilioni 50 kuhakikisha taasisi zinazolisha watu zaidi ya 300 kama magereza na kambi za jeshi zinafungiwa mifumo ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma kutoka REA, Martha Chassama amesema wakala umejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia huku akiendelea kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
“Rais amekuwa ni kinara katika kuhakikisha anaokoa Watanzania waliokuwa wanafariki au kupata madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia. Na sisi REA tutaendelea kuhakikisha tunatoa elimu kwa umma ili lengo la kuhakikisha kufikia 2034 asilimia 80 au zaidi ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema.
Awali mpishi wa shule hiyo, Said Ruanda
amesema wakati wanatumia kuni walikuwa wanatumia muda mwingi kuandaa chakula, juwepo wa joto na moshi.
“Kwa kweli kuna utofauti mkubwa sana toka tumeanza kupikia kwa kutumia gesi. Jikoni hamna moshi sana kama tulivyokuwa tunapikia kwa kuni lakini pia unaweza kupika ukiwa na nguo zako ulizokuja nazo na usichafuke tofauti na hapo zamani ilikuwa lazima ubadilishe nguo uvae nguo nyingine ili nguo zako ulizokuja nazo zisichafuke,” amesema.