Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MWENDESHAJI Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Hiari (WRF), Muchunguzi Kabonaki ameishauri jamii kujiunga na mfuko huo iweze kunufaika nao.
Mfuko huo upo Chini ya Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Kabonaki ametoa ushauri huo alipozungumza na Gazeti la MFANYAKAZI akielezea jinsi mwanachama atakavyonufaika.
Amesema WRF unatoa mafao ya aina tano mojawapo likiwa ni fao la kustaafu.
“Mwanachama aliyefikisha umri wa kisheria wa kustaafu kuanzia miaka 55 anapewa mafao, jumla ya michango yake na faida kwa kipindi alichokuwa mwanachama,” amesema.
Fao lingine linalotolewa na mfuko huo ni la kujitoa. Katika hilo Kabonaki amesema mwanachama aliyeamua kujitoa atapewa michango yake yote pamoja na faida zilizopatikana.
“Mwanachama anapojisajili kwenye mfuko hadi afikishe miaka miwili ndio ataruhusiwa kujitoa.
“Faida zinazopatikana za kiuwekezaji kila robo mwaka zitapelekwa kwenye akaunti yake,” amesema.
Kabonaki ameelezea fao lingine ni la kukosa kazi, kwamba mwanachama aliyepoteza kazi atapewa michango yake pamoja na faida.
Amesema mwanzo atapewa asilimia 50 kwa miezi mitatu ya kwanza, akiendelea kukosa kazi kwa miezi sita atapewa sehemu iliyobaki.
“Mfuko pia unatoa huduma ya “annuity”. Huu ni utaratibu ambao mwanachama ataweka fedha zake kwa mkupuo na kuingia makubaliano ya kulipwa kidogo kidogo kwa kipindi maalum. Katika kipindi hicho fedha ya mwanachama itaendelea kuzalisha faida kutoka kwenye uwekezaji ambao mfuko unafanya,” amesema.
Vile vile amesema kuna fao la wategemezi. Akifafanua hilo amesema wategemezi wa mwanachama aliyefariki watalipwa kulingana na kiwango kilichopo kwenye akaunti ya mwanachama pamoja na faida zote.
“Pia kuna manufaa ya kutumia michango ya mwanachama kama dhamana kwa ajili ya mikopo benki,” amesema.
Mfuko huo umeanzishwa mwaka jana kwa lengo la kutoa hifadhi ya jamii ya nyongeza kwa wanachama wa sekta rasmi na isiyo rasmi.