Na Lucy Lyatuu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kuzindua boti nne za kisasa za doria katika eneo la majini ili kudhibiti vitendo viovu vya uingizwaji wa bidhaa hatarishi pamoja na kulinda mapato ya nchi.
Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano TRA,Richard Kayombo amesema hayo leo Dar es Salaam na kuongeza kuwa uzinduzi huo utafanyika Septemba 18,2024 jijini Mwanza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko.
Kuhusu uzinduzi huo amesema itakwenda pamoja na utoaji wa taarifa ya kuanza Kwa boti hizo Kwa ajili ya kudhibiti magendo na boti hizo zitaelekezwa kwenye maziwa yote nchini na baharini.
Amesema boti hizo zitasaidia tatizo la upotevu wa mapato uingizwaji wa bidhaa za magendo lakini pia upitishwaji wa bidhaa zisizotakiwa kutoka nchini.
” Boti zitasaidia kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizokubalika, uingizwaji wa bidhaa hatarishi pamoja na kupitisha bidhaa zisizotakiwa”‘ amesema Kayombo na kuongeza kuwa zitasambazwa katika bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Kigoma.
Amesema kutokana na matumizi ya boti hizo, TRA inatoa tahadhari kwa wanaohusika na magendo kuepukana na vitendo hivyo.
Amesema Mamlaka ya Mapato linasimamia suala la Ulinzi na usalama wa majini ili vitu hatarishi ama wahamiaji haramu wasisingie nchini au bidhaa kutoka bila utaratibu.
Kayombo amesema kupitia uzinduzi huo, wanafanya vitendo hivyo viovu wake chonjo kwani TRA inaongezeka udhibiti wa uingizwaji wa bidhaa hatarishi au zisizopitia mikono ya udhibiti salama.