Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi iendelee kulisimamia kwa karibu Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuhakikisha huduma za treni ya SGR zinaboreshwa na miundombinu inaimarishwa ili mradi huo uweze kudumu kwa muda mrefu.
Majaliwa amesema hayo leo wakati akiahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge jijini Dodoma.
Amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendeleza sekta ya uchukuzi kwa kusimamia sekta ya reli ikiwemo ujenzi wa SGR na uendeshaji wa treni ya kisasa ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.
Amesema Desemba 31, mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza kuanza uendeshaji wa reli ya SGR kwa kipande cha Dar es Salaam – Dodoma ifikapo mwezi Julai, mwaka huu.
“Naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa, safari za treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam – Morogoro zilianza Juni 14 mwaka huu, 2024.
“Julai 25, 2024 uendeshaji wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ulianza.” amesema.
Ameongeza kuwa, Agosti mosi mwaka huu, Samia Suluhu Hassan alizindua utoaji wa huduma za reli ya kisasa ya SGR kutoka jiji la Dar es salaam kupitia Mkoa wa Morogoro hadi Jiji la Dodoma.
Amesema treni hiyo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi na imechangia kuimarisha sekta ya usafirishaji. “Kipekee ninaomba kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia maono yake na kwa kweli anaahidi, anatekeleza, Kazi Iendelee”.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie kwa ukaribu upatikanaji na usambazi wa pembejeo za kilimo hususani mbolea ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa kilimo na kwa kuzingatia jiografia za kanda za kilimo nchini.