Na Mwandishi Wetu
WAZIRIi wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amewaagiza maofisa kazi kote nchini, kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutoa taarifa kwa wakati za wafanyakazi wanaoumia maeneo ya kazi ili waweze kupewa stahiki zao kama Sheria inavyotaka.
Ridhiwan ametoa agizo hilo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili baina ya WCF na maofisa kazi kutoka mikoa ya Tanzania Bara.
Ridhiwan pia amewaagiza maofisa kazi hao kusimamia sheria za kazi kwa kufanya kaguzi mahala pa kazi ili kuhakikisha waajiri wanatekeleza matakwa ya sheria ya fidia kwa wafanyakazi.
“Jukumu lenu maofisa kazi ni kusikiliza malalamiko na kwa shughuli zinazohusu WCF jukumu lenu ni kuandika na kutoa taarifa WCF,
“Sio kugeuka washauri wa waajiri ili kudhulumu haki za wafanyakazi,”amesema na kuongeza: “andikeni vitu ambavyo mwisho wa siku wafanyakazi watapata haki zao na sio kuandika ili sheria ionekane haifai,” amesema.
Aidha Ridhiwan amewataka maofisa kazi hao kusoma na kuelewa vizuri muswada wa mabadiliko ya sheria ya huduma za jamii, 2024 ambayo inahusu pia mabadiliko katika sheria ya fidia kwa wafanyakazi ili waweze kuwa wasisimamizi wazuri wa sheria hiyo mara baada ya kuwekwa sahihi na Rais.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt John Mduma amesema kwamba Mfuko umejizatiti katika kuhakikisha huduma zake zinapatikana kupitia mtandao pamoja na kuimarisha ushirikiano na Idara ya Kazi kupitia maofisa kazi hao kwa lengo la kuhakikisha kiwango cha ukidhi wa uzingatiaji wa sheria ya fidia kwa wafanyakazi kinaongezeka.
“Kwa sasa huduma zetu kwa zaidi ya asilimia 90 zinapatikana mtandaoni, lakini pia tumekuwa tukishirikiana vizuri na wenzetu wa Idara ya Kazi kupitia maofisa kazi hawa ambao kiukweli ushirikiano huu umesaidia ‘compliance’ kwa upande wetu,” amesema.
Naye Kamishna wa kazi nchini, Suzan Mkangwa amesema Ofisi yake imekuwa ikishirikiana na WCF kuhakikisha malalamiko ya wafanyakazi wanaoumia au kupata ugonjwa unaotokana na kazi zao yanatatuliwa kwa wakati.
Maofisa kazi 78 kutoka mikoa yote ya Tanzania bara wamehudhuria kikao kazi hicho.