Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAKULIMA wameishukuru Kampuni ya Pass Leasing kwa kuweza kuwadhamini mikopo ya matrekta, gari la kubeba mizigo na vifaa vingine.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo, katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, amesema
kilimo ni uti wa mgongo isiwe kwa maneno bali iwe kwa vitendo.
Amesema wakulima wanaendelea kuelewa umuhimu wa kutumia vifaa vya kisasa
Ikiwa ni pamoja na kuamini juhudi kubwa zinazofanywa na serikali.
Amesema wamegawa trekta 12, gari moja la kubebea mizigo, mashine ndogo ya kuchakata mazao ikiwa ni katika kuleta mabadiliko makubwa kwa watumiaji wa zana za kilimo waliokuwa wanalima kwa mkono
Amesema faida ya kutumia trekta itamwezesha mkulima kulima eka nyingi kwa wakati mmoja, pia hawatalima mashamba yao pekee bali na ya wengine katika maeneo yao kwa kuwakodisha.
“Nawapongeza sana kampuni ya Pass Leasing kwa utashi huu mkubwa mlio nao na mmedhamiria kusaidia kundi hili la wakulima ambalo ndilo kundi kubwa la Watanzania, niwapongeze sana kwasababu serikali inaanzisha mpango lakini inafanya kazi na wadau mbalimbali ili kufikia malengo yake,” amesema.
Amesema hayo wanayoyafanya ni wazi kwamba wamemwelewa vizuri Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo kwa kufanya hivyo wameyapa maonyesho hayo thamani.
Amewataka wakulima waliokabidhiwa vifaa hivyo wavitumie kwa uangalifu ili iwe faida kwao na kwa wengine.
Naye mnufaika Minza Mlela ameishukuru kampuni ya Pass Leasing kwa kumkubadhi trekta ambayo itaenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kumrahisishia kazi zake.