Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM; MTEGO wa kisasa wa nzi wa maembe umebuniwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), wenye uwezo wa kupiga picha, kuzichakata, kutambua aina ya mdudu ikiwa ni pamoja na kuhesabu wadudu walionaswa.

Mhadhiri kutoka Idara ya Mawasiliano Angani DIT, Dkt. Mbazingwa Mkiramweni amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa habari hii.
Dkt. Mkiramweni amesema, “Mtego tulioutengeneza unakamata wadudu na kuwaua kama ambavyo sasa hivi wakulima wanatumia mtego wa makopo ya kawaida kwa kuweka dawa inayovutia nzi hao umbali wa mita 100 kutoka mtego ulipo.

“Kwa hiyo mtego wetu unapiga picha mara mbili kwa siku. Utapiga mchana na kuhesabu umekamata wadudu wangapi. Utapiga na jioni utahesabu vile vile.
” Kisha idadi iliyopatikana inatumwa kupitia teknolojia . Unaweza kuona taarifa hiyo popote ulipo kupitia simu au komputa ukiunganisha mtandao,” amesema.
Amesema teknolojia hiyo waliyoibuni inaweza kunyumbulisha na kuonyesha kwa siku wadudu wamepatikana wangapi, kwa wiki, kwa mwezi hata kwa mwaka.
Amesema wametafiti mtego huo kwa kuwa nzi hao wamekuwa wakiharibu maembe na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima na taifa.

Kwani wakulima hushindwa kufanya biashara ndani na nje ya nchi kwa sababu ya uharibifu unaofanywa na nzi hao.