Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Tanzania inaendelea kujenga amani na utulivu huku Serikali ikiendelea kutekeleza miradi ya maendeleo na ahadi ilizotoa kwa wananchi licha ya changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Amesema ni muhimu kutofautisha dhana ya amani na utulivu, akieleza kuwa ingawa nchi ilikumbana na changamoto wakati wa uchaguzi, juhudi maalumu zimefanyika kurejesha hali ya amani na kuendelea kuimarisha utulivu.
Akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya Serikali, amesema Rais ameendelea kuelekeza utekelezaji wa ahadi kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati na huduma za kijamii.
Ametaja Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa, ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.
Amesema kabla ya mradi huo, uwezo wa uzalishaji umeme nchini ulikuwa takribani megawati 1,700, hivyo kukamilika kwake ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa nishati.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na miradi mingine ya maendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwamo bandari, afya, elimu na maji.
Kuhusu uchumi, amesema Serikali imeendelea kusisitiza kujitegemea kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kugharamia shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, amekiri kuwa kipindi hicho kimekuwa na changamoto, akisisitiza kuwa viongozi nao ni binadamu wanaopitia nyakati ngumu, hivyo mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kutazamwa sambamba na changamoto zilizojitokeza.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!