Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 16

Dkt Nungu: Fursa Za Ubunifu Zipo Kwa Watanzania Wote Bila Kujali Elimu

Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM: Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inaendelea kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuendeleza ubunifu wao kupitia mafunzo, ushauri wa kitaalamu, ruzuku, mikopo na kuwaunganisha na wawekezaji, kwa lengo la kukuza biashara na kuongeza ajira nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alieleza hayo Oktoba 8, 2026, katika kipindi cha “Konekti na Waziri – Tushauri Tutekeleze”, kilichoendeshwa na Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, kupitia mitandao ya kijamii ya YouTube, Facebook na Instagram.

Kipindi hicho kilijadili fursa za uwezeshaji kwa vijana katika ubunifu na teknolojia, huku washiriki wakipata nafasi ya kuuliza maswali kuhusu upatikanaji wa mitaji, masharti ya mikopo, gharama za leseni na namna ya kuingiza bidhaa zao sokoni.

Dkt. Nungu alisema COSTECH inatumia mifumo mbalimbali kuwawezesha wabunifu katika hatua tofauti za maendeleo ya mawazo, bidhaa na biashara zao. Mifumo hiyo ni pamoja na Buni Innovation Hub, Dar Teknohama Business Incubator (DTBI), Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji Teknolojia (CDTT) na Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia (MTUSATE).

Msimamizi wa Buni Innovation Hub na DTBI, Patience Abraham Karua, alisema Buni huwasaidia wabunifu walio katika hatua za awali kuendeleza mawazo yao na kutengeneza bidhaa ya awali inayofanya kazi (MVP), kupitia ushauri wa kitaalamu unaotolewa kwa kipindi cha miezi mitatu.

Alisema DTBI, kwa upande mwingine, huwasaidia wabunifu ambao tayari wana bidhaa zilizokamilika kuziingiza sokoni kupitia ushauri wa kibiashara na kuwaunganisha na wawekezaji.

Karua alisisitiza kuwa fursa hizo zipo kwa Watanzania wote bila kujali kiwango cha elimu. Alitaja Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kuwa miongoni mwa mifumo inayowapa nafasi wabunifu kutoka shule, vyuo na sekta isiyo rasmi kuendeleza mawazo yao.

Kwa mujibu wa Ofisa Mwandamizi wa MTUSATE, Ntufye Mwakigonja, kupitia MAKISATU, mfuko huo umefikia wabunifu zaidi ya 3,000 nchini, kuwawezesha takribani 400 na kusaidia kuanzishwa kwa kampuni changa 75.

Mwakigonja alisema COSTECH, kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, ilianzisha Dirisha la Ubiasharishaji wa Matokeo ya Tafiti na Ubunifu mwezi Aprili 2025. Dirisha hilo linalenga kuwawezesha wabunifu kupata mikopo kwa kutumia dhamana ya COSTECH.

Alieleza kuwa, kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa, vijana 10 walikuwa wamepata mikopo yenye thamani ya jumla ya Sh bilioni moja kupitia utaratibu huo.

WABUNIFU WANAVYOZIGEUKA FURSA KUWA BIASHARA

Katika kipindi hicho, wanufaika wawili wa programu za COSTECH, walioanzisha kampuni za Novfeed na Imara Tech, walieleza namna walivyotumia fursa za uwezeshaji kukuza biashara zao.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Novfeed, Diana Orembe, alisema alipata ruzuku ya Sh milioni 10 kupitia COSTECH na DTBI baada ya kuwasilisha maombi mtandaoni na kushiriki mchakato wa ushindani mbele ya majaji.

Alisema kampuni hiyo, iliyosajiliwa mwaka 2020, imekua na kufikia hatua ya kuwa na kiwanda chenye uwezo wa kuzalisha tani 6,000 za chakula cha samaki kwa mwaka, pamoja na mbolea ya kikaboni inayojulikana kama Ecovita.

Kwa mujibu wa Orembe, kampuni hiyo ina thamani ya zaidi ya Sh milioni 100, imeajiri vijana 20 na kuhudumia wakulima na wafugaji zaidi ya 3,000.

Kwa upande wake, mwanzilishi wa Imara Tech ya Arusha, Alfred Chengula, alisema alipata ruzuku ya Sh milioni 20 kwa ajili ya majaribio ya ubunifu wake, na baadaye Sh milioni 40 kupitia MAKISATU.

Alisema fursa ya kushiriki jukwaa la kibiashara nchini Finland ilimwezesha kupata mwekezaji wa kimataifa aliyesaidia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa kampuni hiyo.

Chengula alisema uwezo wa uzalishaji wa Imara Tech uliongezeka kutoka mashine 10 hadi 60 ndani ya siku 15. Aliongeza kuwa kampuni hiyo ina wafanyakazi 18 wa moja kwa moja na husafirisha mashine zake katika nchi nane za Afrika.

VIJANA WATAKIWA KUFUATILIA FURSA

Akizungumza katika kipindi hicho, Waziri Nanauka aliwahimiza vijana kufuatilia taarifa za fursa za uwezeshaji na kuwasilisha maombi yao kwa umakini ili waweze kunufaika na programu zilizopo.

Pia alieleza kuhusu nafuu ya kodi ya mapato kwa kampuni changa zinazokidhi vigezo katika mwaka wao wa kwanza wa biashara, akisema hatua hiyo inalenga kuzipa nafasi ya kukuza mitaji na kuimarisha shughuli zao.

Waziri huyo aliwataka vijana kujisajili katika mfumo wa Youth Empowerment System (YES) na kutumia jukwaa la Vijana Connect kupitia tovuti ya https://portal.vijana.go.tz kupata taarifa za fursa za mikopo, masomo na fursa za kimataifa zinapotangazwa.

Akijibu maswali ya vijana kuhusu upatikanaji wa fedha, Dkt. Nungu alifafanua kuwa ruzuku na mikopo vina masharti tofauti. Alisema baadhi ya ruzuku hutolewa kwa kuzingatia ubora wa ubunifu, huku mikopo ikihitaji tathmini ya uwezo wa biashara kuzalisha mapato na kurejesha fedha kwa mujibu wa miongozo ya benki.

Aidha, alisema COSTECH inashirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutoa mafunzo na usaidizi wa kulinda haki miliki za wabunifu.

Aliongeza kuwa COSTECH pia huwasaidia baadhi ya wabunifu kuunganishwa na taasisi pamoja na wateja wa kimkakati ili kufanya majaribio ya bidhaa zao na kupata fursa za kuziboresha.

Kwa upande wake, Waziri Nanauka alisema Serikali iko tayari kupokea maoni kuhusu nyaraka na taratibu zinazowakwamisha vijana kupata fursa za uwezeshaji, ili changamoto hizo ziweze kufanyiwa kazi.

Kipindi hicho kililenga kuongeza uelewa wa vijana kuhusu fursa zilizopo katika ubunifu na teknolojia, pamoja na kuwahamasisha kutumia mifumo ya uwezeshaji iliyopo kugeuza mawazo yao kuwa biashara zinazoweza kuzalisha ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.