Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 14

VETA Yaweka Mikakati Kupunguza Vikwazo Kwa Vijana Wenye Ulemavu

Na Lucy Ngowi

RUKWA: MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeweka mikakati ya kuwawezesha vijana wenye ulemavu kupata fursa sawa za mafunzo, ikiwemo kuboresha miundombinu ya vyuo, kutoa vifaa saidizi na kuwajengea uwezo walimu kuwahudumia kulingana na mahitaji yao.

Meneja wa Uhusiano na Masoko wa VETA, Sitta Peter, amesema hayo wakati akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayoendelea mkoani Rukwa, akieleza hatua zinazochukuliwa na mamlaka hiyo kuhakikisha ulemavu hauwi kikwazo kwa vijana kupata ujuzi wa ufundi stadi.

Habari Picha 14042

Mwalimu wa Ushonaji VETA Songea, Riziki Ndumba akiwa na Meneja wa Uhusiano na Masoko wa VETA, Sitta Peter,

Amesema VETA inaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo kwa kuhakikisha karakana, mabweni na maeneo mengine ya vyuo yanakuwa rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu ili waweze kujifunza na kuishi chuoni bila kukabiliwa na vikwazo vinavyoweza kuepukika.

Habari Picha 14043Meneja wa Uhusiano na Masoko wa VETA, Sitta Peter, akiwa na Mwanafunzi wa ushonaji kutoka VETA Nkasi, Imelda Kanyengele

Kwa mujibu wa Sitta, mikakati hiyo pia inahusisha kuwajengea uwezo walimu na watumishi wa vyuo kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ikiwemo matumizi ya lugha ya alama, maandishi ya nukta nundu (Braille) na vifaa saidizi vinavyorahisisha ufundishaji na ujifunzaji.

Amesema mamlaka hiyo pia imekuwa ikiwasaidia baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo wanaokabiliwa na changamoto za usafiri, ikiwemo kuwawezesha kupata vifaa vya usafiri vinavyorahisisha safari zao za kwenda na kutoka chuoni.

Habari Picha 14044

Mhitimu wa VETA Tanga, Ernest Igoboko akiwa na Meneja wa Uhusiano na Masoko wa VETA, Sitta Peter

Ametoa mfano wa Riziki, mhitimu wa Chuo cha VETA Songea, ambaye alikabiliwa na changamoto ya usafiri kutoka nyumbani kwenda chuoni, hali iliyohitaji msaada ili kurahisisha upatikanaji wa mafunzo.

Sitta amesema serikali hugharamia ada za mafunzo kwa wanafunzi hao, ingawa baadhi yao bado hukabiliwa na mahitaji mengine kama nauli na vifaa vya karakana, ikiwemo viatu na mavazi maalumu ya kujikinga wakati wa mafunzo.

Habari Picha 14045

Meneja wa Uhusiano na Masoko wa VETA, Sitta Peter, akimwangalia Mhitimu wa VETA Songea, Gonsalva Lungu (aliyeko katikati), akiwa anapima nguo

Amesisitiza kuwa VETA itaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha vijana wenye ulemavu wanapata fursa sawa za kujifunza, kupata ujuzi na kutumia maarifa yao kujiajiri au kuajiriwa.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.