Wahamasishwa kujiunga ili kulinda mitaji yao
Na Mwandishi Wetu, Geita
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewahimiza wananchi hususan wajasiliamali mkoani Geita kujiunga na Bima ya Afya kupitia Kifurushi cha Umoja Afya ambacho kimeandaliwa kwa lengo la kuwawezesha kujinga na kuwa na uhakika wa matibabu wakati wowote.
Aidha imeelezwa kuwa, kujiunga na bima ya afya kutawawezesha kulinda afya zao pamoja na mitaji ya biashara zao bila kuathirika na gharama za matibabu endapo watakumbwa na maradhi.
Ujumbe huo umetolewa katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, ambako NHIF inatoa elimu kwa wachimbaji, wafanyabiashara, wakulima, mafundi na makundi mengine kuhusu umuhimu wa bima ya afya na namna ya kujiunga.
Meneja wa NHIF Mkoa wa Geita, Sophia Kaku, amesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kuwafikia wananchi kutoka makundi mbalimbali, ikiwamo wachimbaji wadogo na wakubwa, wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga, vyama vya ushirika, vikundi vya kuweka na kukopa (Vikoba), vilabu vya michezo, wakulima na mafundi.
Amesema NHIF imeshiriki pia katika kongamano la mifuko ya hifadhi ya jamii lililowakutanisha wadau kutoka taasisi mbalimbali, zikiwamo NSSF, PSSSF na WCF.
Kaku amesisitiza kuwa, suala la afya ni msingi wa maendeleo ya mtu na familia, kwani ugonjwa unaweza kuathiri uwezo wa kufanya kazi, kipato na ustawi wa kaya, hususan kwa wananchi wanaotegemea shughuli za kila siku kujipatia riziki.
Kutokana na hayo, amewataka kutumia fursa hiyo ili kunufaika na huduma za matibabu katika vituo zaidi ya 10,000 vilivyosajiliwa na NHIF nchini.
Ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi wenye uwezo kuwasaidia watu wenye ulemavu, yatima na makundi mengine yenye uhitaji kwa kuwakatia bima ya afya, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mshikamano wa kijamii na inaweza kuwakinga dhidi ya gharama za matibabu.

NHIF imeendelea kutoa wito kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo kutembelea banda lake ili kupata elimu na ufafanuzi kuhusu huduma zinazotolewa, mipango ya bima iliyopo na taratibu za kujiunga.
Kupitia ushiriki huo, NHIF inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kulinda afya zao, kwa kutambua kuwa afya bora ni msingi wa kuendeleza shughuli za kiuchumi na kujenga ustawi wa familia.
Kwa upande wa wananchi walioshiriki Kongamano hilo, wameipongeza NHIF kwa kuja na Kifurushi cha Umoja Afya ambacho kimezingatia hali ya kipato cha wananchi wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo na hata wasio na shughuli maalum.
“Katika hili NHIF tunawapongeza sana, endeleeni kutufikia wananchi has awa maeneo ya vijijini ili kila mwananchi aweze kuwa na uelewa lakini pia awe na uhakika wa matibabu wakati wote.


Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!