Na Lucy Ngowi
GEITA: BENKI ya Azania imewawekea fursa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kupata mikopo ya hadi Sh. Bilioni tano bila dhamana, kwa kutumia akaunti ya benki hiyo na fedha wanazotarajia kupokea kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Meneja wa Azania Benki Tawi la Geita, Rhoda Baluhya amesema hayo mbele ya Mgeni Rasmi, Naibu Waziri Steven Kiruswa alipotembelea banda lao katika maonesho ya tisa ya Kitaifa ya ya Teknolojia ya madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema benki kupitia bidhaa hiyo maalumu kwa wadau wa sekta ya madini, mteja anaweza kukopeshwa hadi asilimia 80 ya thamani ya fedha anazotarajia kupokea baada ya kuuza madini yake kupitia mfumo unaohusisha Benki Kuu.

Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kuendelea na shughuli zao za uzalishaji na biashara wakati wakisubiri kukamilika kwa taratibu za malipo.
Mbali na mikopo hiyo, amesema benki hiyo inatoa huduma mbalimbali za kifedha kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa sekta ya madini, ikiwamo mikopo ya mitaji, uwekezaji na ununuzi wa mitambo na vifaa vya uzalishaji.
Kwa mujibu wa meneja huyo,, baadhi ya mikopo ya mitaji hutolewa kwa ajili ya kuendesha shughuli za biashara na inaweza kulipwa kwa vipindi vya miezi mitatu, huku mikopo ya uwekezaji ikilenga utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Aidha, amesema benki hiyo inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa mitambo, mashine na vifaa vya uzalishaji, pamoja na vyombo vya usafirishaji kama magari, malori na matipa.
Katika hatua nyingine, amesema benki imeingia makubaliano na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa mikopo yenye riba ya asilimia tano kwa mwaka kwa ajili ya ujenzi wa vituo na maeneo ya huduma za mafuta vijijini.
Benki hiyo imeeleza kuwa pia inatoa mikopo ya uwekezaji ya muda mrefu inayoweza kufikia miaka minane, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, magari na mahitaji mengine yanayowawezesha wawekezaji katika sekta ya madini kuongeza uwezo wa uzalishaji.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!