Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 14

Madini: Kutoka Ushirikina Hadi Sayansi, Wachimbaji Wabadilika

Na Lucy Ngowi

GEITA: SEKTA ya madini mkoani Geita imeanza kuachana na mbinu za jadi zilizowahi kutumiwa na baadhi ya wachimbaji katika kutafuta madini, huku matumizi ya sayansi, maabara na teknolojia za kisasa yakitajwa kuongeza ufanisi na tija katika uchimbaji.

Mabadiliko hayo yameelezwa na Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Madini Mkoa wa Geita, Mshana Jeremiah, wakati viongozi wa sekta hiyo wakiwahamasisha wachimbaji, wanawake na wadau mbalimbali kushiriki Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita.

Jeremiah amesema matumizi ya teknolojia yamekuwa sehemu muhimu ya shughuli za uchimbaji, tofauti na zamani ambapo baadhi ya wachimbaji walitegemea imani na taratibu za kishirikina katika kutafuta madini.

Amesema mabadiliko hayo yanapaswa kuendelezwa kwa wachimbaji kutumia maarifa, sayansi na teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na kuboresha shughuli zao.

Katika hatua nyingine, amesema Oktoba 2, 2026, imetengwa kwa ajili ya kujadili na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika rasilimali za madini na gesi kupitia dhana ya Local Content.

Amesema siku hiyo itawakutanisha viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya madini, akiwemo Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), John Wambura.

Aidha, amesema Mchungaji Bonifas Mwamposa anatarajiwa kushiriki maonyesho hayo kama mmoja wa wachimbaji, huku Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akitarajiwa kushiriki katika semina na kukutana na wachimbaji kusikiliza changamoto zao na kutoa miongozo kuhusu shughuli za uchimbaji.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Mwanamke na Madini, Rehema, amewataka wanawake wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa madini, mkoani Geita na maeneo mengine, kujitokeza kwa wingi katika semina na shughuli mbalimbali za maonyesho hayo.

Amesema ushiriki wa wanawake ni muhimu katika kuhakikisha wanatumia fursa zinazopatikana katika sekta ya madini na kunufaika katika mnyororo wa thamani.

Maonyesho hayo yanaendelea kuwa jukwaa la kukutanisha wachimbaji, wataalamu, wawekezaji na wadau wengine wa sekta ya madini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, teknolojia na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.