Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 15

Waziri: Bila Takwimu, Mipango Ya Maendeleo Haiendi

Na Lucy Ngowi
GEITA:  WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema takwimu sahihi ni msingi wa Serikali kufanya maamuzi na kupanga mipango ya maendeleo inayozingatia hali halisi ya Taifa.
Sangu amesema hayo alipotembelea Banda la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika Maonyesho ya Tisa ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Amesema NBS ina jukumu muhimu la kukusanya, kuchambua na kutunza takwimu zinazowezesha Serikali na wadau wengine kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
Habari Picha 13813
“NBS wanafanya kazi nzuri, bila wao hakuna mipango inaenda,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, upatikanaji wa takwimu kwa wakati unaiwezesha Serikali kutambua mahitaji ya wananchi, kuweka vipaumbele na kuchukua hatua zinazolingana na uhalisia wa maeneo mbalimbali nchini.
Amesisitiza umuhimu wa NBS kuendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, uchambuzi na utunzaji wa takwimu ili ziweze kutumika ipasavyo katika maamuzi ya kitaifa.
Sangu pia ameipongeza NBS kwa kushiriki katika maonyesho hayo, akisema ushiriki huo unatoa fursa kwa wananchi na wadau kuelewa kazi za taasisi hiyo na namna takwimu zinavyotumika katika sekta mbalimbali za uchumi.
Amesema kazi ya NBS ni sehemu muhimu ya safari ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kuweka msingi wa maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya Watanzania.
Ameitaka NBS kuendelea kuhakikisha Serikali inapata takwimu sahihi na kwa wakati ili ziweze kutumika katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa.
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.