Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 13

VETA Yawahamasisha Vijana Kujikita katika Elimu ya Ufundi

Na Lucy Ngowi

MWANZA: VIJANA wametakiwa kutumia fursa zinazotolewa na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kwa kujifunza taaluma mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha kujiajiri au kupata ajira na kujenga maisha yao.

Akizungumza katika Maonesho ya tisa ya Kitaifa yaTenolojia ya Madini, yaliyofanyika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Geita, Musa Doma ambaye ni Mkufunzi wa Umeme kutoka VETA Mwanza, amesema ushiriki wao unalenga kutoa elimu kwa wananchi, hususan vijana, kuhusu fursa zinazopatikana kupitia mafunzo ya ufundi.

Habari Picha 13821

Doma amesema katika maonyesho hayo wanawakilisha mafunzo ya umeme wa viwandani na migodini, huku wakitoa ufahamu kuhusu umuhimu wa vijana kupata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Amesema elimu ya ufundi ina nafasi kubwa katika kuwawezesha vijana kutumia ujuzi wao kujiajiri, kuajiriwa katika taasisi na kampuni mbalimbali, pamoja na kuanzisha shughuli zao za uzalishaji.

“Tunawahamasisha vijana waje VETA, wajifunze ufundi na kupata ujuzi ambao unaweza kuwasaidia kujiajiri au kuajiriwa. Ufundi ni fursa inayoweza kumwezesha kijana kujenga maisha yake,” amesema Doma.

Ameongeza kuwa, kupitia mafunzo ya ufundi, vijana wanaweza kupata maarifa na ujuzi wa vitendo unaoweza kutumika moja kwa moja katika maeneo ya kazi, hivyo kuwaongezea uwezo wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, VETA inaendelea kutumia maonyesho na shughuli mbalimbali za uhamasishaji kuwafikia vijana na kuwaelimisha kuhusu fursa za mafunzo ya ufundi stadi.

Doma amewataka vijana kutokaa kusubiri ajira pekee, bali kuchangamkia fursa za kujifunza ufundi na kutumia ujuzi huo kujiajiri, kuajiri wengine na kuchangia maendeleo ya jamii.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.