Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 15

AI Yashika Kasi Sera Zinaendana?

Dkt. Nyinondi: Tanzania inahitaji mfumo unaoweza kubadilika kwa kasi ya teknolojia
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA: KASI kubwa ya maendeleo ya Akili Unde (AI) imeibua swali kuhusu uwezo wa sera za Tanzania kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia hiyo, huku Dkt. Philbert Nyinondi akisisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa kisera unaoweza kubadilika kwa wakati.
Habari Picha 13808
Dkt. Nyinondi, Mhadhiri Mwandamizi na mtafiti wa mawasiliano ya sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ametoa hoja hiyo kupitia utafiti unaochunguza uwezo wa sera na mifumo ya uongozi katika elimu ya juu kukabiliana na maendeleo ya haraka ya AI.
Utafiti huo wenye kichwa “Je, Miongozo ya Akili Unde Inaweza Kwenda Sambamba na Kasi ya Maendeleo ya Akili Unde? Tathmini ya Uwezo wa Sera Kubadilika katika Elimu ya Juu Tanzania,” uliwasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Vyuo Vikuu Vitano (5UCC), uliofanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Arusha, Septemba 23 hadi 25, 2026.
Katika utafiti huo, Dkt. Nyinondi amelinganisha Miongozo ya Kitaifa ya Akili Unde katika Elimu (NGAIE, 2025) na Miongozo ya Kitaifa ya Elimu ya Kidijitali kwa Vyuo Vikuu (NDEGU, 2025), akitathmini uwezo wake wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
SERA ZIPO, MWITIKIO JE?
Habari Picha 13806
Utafiti unaonyesha kuwa Tanzania tayari ina msingi wa sera unaotambua umuhimu wa kufuatilia mabadiliko, kupata mrejesho kutoka kwa wadau na kufanya maboresho katika mifumo ya uongozi wa AI katika elimu ya juu.
Hata hivyo, Dkt. Nyinondi amebainisha kuwa bado kuna maeneo ambayo hayajaainishwa kwa uwazi, ikiwamo mazingira yanayopaswa kusababisha mapitio ya haraka ya sera, muda wa kushughulikia changamoto za dharura, mfumo wa kutambua mapema teknolojia zinazoibuka na namna taarifa za ufuatiliaji zinavyoweza kufikishwa katika hatua za maamuzi ya kisera.
Kwa mtazamo huo, hoja kuu ya utafiti si kuwepo au kutokuwepo kwa uwezo wa kubadilisha sera, bali ni namna mfumo huo unavyoweza kuhakikisha mabadiliko yanafanyika kwa wakati unaohitajika wakati teknolojia ikiendelea kubadilika.
Mjadala huo uliungwa mkono na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, wakati akifungua mkutano huo, akisisitiza umuhimu wa Tanzania kuwa na mjadala mpana kuhusu AI na utayari wa nchi kukabiliana na mabadiliko yanayoletwa na teknolojia hiyo.
Alisema mjadala huo haupaswi kuangalia pekee kile ambacho teknolojia inaweza kufanya, bali pia namna taasisi, sera na mifumo ya uongozi inavyopaswa kuitikia fursa na changamoto zinazotokana na maendeleo hayo.
AI ISIISHIE KWENYE TEKNOLOJIA
Mjadala wa Arusha pia uliangalia uhusiano kati ya teknolojia na mahitaji ya jamii.
Profesa Raffaella Cagliano wa Politecnico di Milano, Italia, kupitia mada yake kuhusu “Teknolojia kwa Ajili ya Watu,” amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mazingira ya kijamii na kiuchumi ambako teknolojia inatumika.
Kwa upande mwingine, Profesa Tushar Shinde wa IIT Madras Zanzibar amesisitiza umuhimu wa kujenga AI yenye ufanisi, inayofikika na yenye gharama nafuu, akieleza kuwa mjadala haupaswi kujikita katika kujenga mifumo mikubwa pekee.
Hoja hizo zimeunganisha mjadala wa Arusha katika maeneo matatu muhimu: mahitaji ya jamii, ufanisi wa teknolojia na uwezo wa sera kuendana na mabadiliko.
Kwa Tanzania, mjadala huo una umuhimu katika elimu ya juu ambako AI inaendelea kutumika katika ufundishaji, ujifunzaji, tathmini, utafiti na huduma za kitaaluma.
Habari Picha 13809
Wakati Tanzania ikiendelea na tafakuri ya miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), utafiti huo unaibua swali la msingi kuhusu miaka ijayo: Je, mifumo ya kitaifa inaweza kujifunza na kubadilika kwa kasi inayolingana na mabadiliko ya teknolojia?
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.