Na Mwandishi Wetu, Mafia – Pwani
ZAIDI ya wananchi 3,000 wa Kisiwa cha Jibondo, Wilaya ya Mafia, Mkoa wa Pwani, wanatarajiwa kuanza kunufaika na huduma ya umeme baada ya Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika kisiwa hicho wenye thamani ya Sh bilioni 8.4.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba 2026, ambapo kwa sasa umefikia asilimia 82 ya utekelezaji na unatarajiwa kubadilisha maisha ya wananchi kwa kufungua fursa mpya za kiuchumi, kuongeza shughuli za uzalishaji na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

Wananchi hai wameeleza kuwa kwa muda mrefu, wakazi wa Jibondo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli zao za kiuchumi, hususani zinazohusisha uvuvi, uchakataji na uhifadhi wa mazao ya bahari.
Wananchi wanasema kukosekana kwa umeme kuliwafanya kushindwa kutumia fursa mbalimbali za kuongeza thamani ya mazao yao na kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata samaki na bidhaa nyingine za baharini.

Hata hiyo wamesema uwepo wa umeme sasa unakwenda kuleta matumaini mapya, huku wakitarajia kuanzisha biashara na shughuli za uzalishaji zitakazowaongezea kipato, kuunda ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
“Kabla ya umeme wananchi wa Kata ya Jibondo na kisiwa hiki walikuwa katika mazingira magumu sana kwani walikosa baadhi ya fursa za kiuchumi kwa sababu hawakuwa na umeme. Tunaipongeza TANESCO kwa kutuletea umeme; fursa mbalimbali zinafunguka na uchumi utazidi kukua,” amesema Hassan Mohamed, Diwani wa Kata ya Jibondo.

Meneja wa TANESCO Wilaya ya Mafia, Seif Kijanga, amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kusambaza umeme, ikiwemo laini kubwa na ndogo za umeme, ufungaji wa mashine umba (transfoma) pamoja na nyaya za kusafirisha umeme baharini kutoka Kisiwa cha Juani hadi Jibondo.
Amesema kazi kubwa iliyobaki ni kulaza nyaya hizo baharini na kwamba zoezi hilo likikamilika, wananchi wataanza kupata huduma ya umeme.


“Mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 82 na unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 3,000 katika kisiwa hiki. Gharama ya mradi ni Sh bilioni 8.4 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba 2026,” amesema Kijanga.


