June 5, 1965: Mwalimu Nyerere akiwa
na aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Taifa la China, Komredi Zhou Enlai katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam ambapo Zhou Enlai, ambapo alitoa hotuba kwa wakaazi wa Dar es Salaam.
Wei Yuanyuan na Li Hongfeng, Beijing Foreign Studies University
MIAKA 50 imepita tangu kifo cha Hayati Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa China, Zhou Enlai, lakini urafiki wake na Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, unaendelea kuwa sehemu muhimu ya historia ya uhusiano wa Tanzania na China.
Miaka 50 iliyopita, Watanzania walipopokea taarifa za kifo cha Zhou Enlai, walijawa na huzuni kubwa. Urafiki wa dhati kati ya viongozi hao wawili uliweka msingi imara wa uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na China, urafiki ambao umeendelea kuvuka vizazi.
1965: MWAKA ULIOBADILI HISTORIA YA TANZANIA NA CHINA
Mwaka 1965 ulikuwa wa kihistoria katika uhusiano wa Tanzania na China. Mwalimu Nyerere alifanya ziara yake ya kwanza nchini China, Mkataba wa Urafiki kati ya nchi hizo mbili ukasainiwa, na baadaye Zhou Enlai akafanya ziara rasmi nchini Tanzania.
Mnamo Februari 1965, Mwalimu Nyerere alizuru China kwa mara ya kwanza. Alitembelea viwanda na miradi ya ushirika wa umma katika miji ya Beijing, Nanjing na Shanghai.
Katika ziara hiyo, Nyerere aliwasilisha rasmi ombi kwa viongozi wa China la kusaidia kujenga reli itakayounganisha Tanzania na Zambia, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya nchi hizo mbili.
Wakati huo, China yenyewe ilikuwa bado ikikabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kimaendeleo.
Hata hivyo, baada ya kusikia ombi la Tanzania, Hayati Mwenyekiti Mao Zedong na Waziri Mkuu Zhou Enlai walikubali kusaidia ujenzi wa reli hiyo, iliyokuja kujulikana kama TAZARA.
Zhou Enlai aliahidi kuwa baada ya reli kukamilika, umiliki na mamlaka yake vingekuwa mikononi mwa Tanzania na Zambia. China ingetoa teknolojia, utaalamu na uzoefu wake ili kusaidia nchi hizo kujenga uwezo wa kujiendeleza.
Hayati Profesa Shen Zhiying, mwanzilishi wa taaluma ya Kiswahili nchini China na aliyekuwa mkalimani wa Kiswahili wa Zhou Enlai, alisema Nyerere aliguswa sana na jibu hilo.
Kabla ya hapo, Nyerere alikuwa ameomba msaada wa ujenzi wa reli hiyo mataifa kadhaa ya Magharibi, lakini ombi lake halikupata majibu aliyoyatarajia.
China, licha ya kukabiliwa na changamoto zake za kiuchumi, iliamua kutoa msaada huo.
ZHOU ENLAI TANZANIA: LUGHA ILIYOUNGANISHA MIOYO
Juni mwaka huohuo, Zhou Enlai alifanya ziara rasmi nchini Tanzania. Ilikuwa mara ya kwanza kwa kiongozi wa Jamhuri ya Watu wa China kutembelea Tanzania, ikiwa pia ni ishara ya kuitikia urafiki ulioonyeshwa na Nyerere.
Ujumbe wa China ulipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, ulikaribishwa kwa shangwe kubwa.
Baada ya kuwasili, mkutano mkubwa wa hadhara wa kuwakaribisha viongozi hao ulifanyika katika uwanja wa michezo jijini Dar es Salaam.
Zhou Enlai alitoa hotuba huku Profesa Shen Zhiying akiwa mkalimani.
Hotuba hiyo ilipotafsiriwa kwa Kiswahili, wananchi waliipokea kwa shangwe. Filimbi zilipigwa, ngoma zikapigwa, kofia na nguo zikirushwa juu huku wananchi wakipaza sauti,
“China! China! Zhou Enlai! Zhou Enlai!”
Shangwe hizo zilikatiza hotuba mara kadhaa.
Mwalimu Nyerere alieleza kuwa hakukuwa na kiongozi wa nchi ya kigeni aliyewahi kuheshimiwa na Watanzania kama Zhou Enlai. Moja ya sababu, alisema, ilikuwa hotuba yake nzuri iliyogusa mioyo ya wananchi na ukweli kwamba ilitafsiriwa kwa Kiswahili, lugha waliyoielewa Watanzania.
Kwa Nyerere, lugha haikuwa tu chombo cha mawasiliano, bali daraja la kuunganisha watu na kujenga ukaribu wa kweli.
Hata wakati ujumbe wa China ulipowasili Ikulu, ulipokelewa kwa namna ya pekee. Wajumbe hao waliingia kupitia mlango wa nyuma, jambo lililowashangaza.
Maofisa wa Tanzania waliwaeleza kuwa kwa mila na desturi, wageni hupokelewa kupitia mlango wa mbele, huku familia ikiingia kupitia mlango wa nyuma. Kwa kuwa China ilionekana kuwa ndugu wa dhati wa Tanzania, Wachina walipokelewa kama familia.
Jambo hilo liliwagusa sana wajumbe wa China.
Katika maandalizi ya ziara hiyo, Zhou Enlai alisisitiza matumizi ya Kiswahili kama ishara ya heshima kwa lugha na utamaduni wa Afrika—jambo lililosaidia zaidi kujenga uhusiano wa karibu kati ya watu wa Tanzania na China.
TAZARA: RELI YA UHURU NA URAFIKI
Baada ya ziara yake nchini Tanzania, Zhou Enlai aliendelea kufuatilia kwa karibu suala la ujenzi wa reli ya TAZARA.
Mwaka 1967, China, Tanzania na Zambia zilisaini makubaliano ya ujenzi wa reli hiyo. Ujenzi ulianza rasmi mwaka 1970 na mwaka 1976 reli hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,800 ilikamilika na kuanza kufanya kazi.
Ujenzi wake haukuwa rahisi.
Maelfu ya wahandisi, mafundi na wafanyakazi kutoka China walifika Afrika na kufanya kazi pamoja na wenzao kutoka Tanzania na Zambia, bega kwa bega, katika mazingira magumu. Baadhi yao walipoteza maisha wakati wa kutekeleza jukumu hilo.
Kutokana na mchango huo, reli hiyo ilisifiwa kama Reli ya Uhuru na Reli ya Urafiki.
TAZARA haikuwa reli ya kusafirisha watu na bidhaa pekee. Ilikuwa alama ya mshikamano, ushirikiano na kujitoa kwa pamoja katika kujenga maendeleo.
Hadi leo, reli hiyo inaendelea kuwa sehemu muhimu ya historia ya uhusiano kati ya Tanzania, Zambia na China.
URAFIKI ULIOVUKA NUSU KARNE
Katika maisha yake yote, Mwalimu Nyerere alijitolea kuendeleza uhusiano kati ya Tanzania na China. Alifanya ziara nchini China mara 13, na kuwa miongoni mwa viongozi wa kigeni waliotembelea China mara nyingi zaidi.
Urafiki wake na Zhou Enlai ukawa msingi muhimu katika historia ya uhusiano kati ya Tanzania na China.
Mwaka 1997, wakati Hong Kong iliporejea chini ya mamlaka ya China, Nyerere akiwa katika umri mkubwa, bado alisafiri kwenda kushuhudia hafla ya makabidhiano na kutoa salamu na pongezi zake kwa wananchi wa China.
Leo, viongozi hao wawili wamefariki dunia, lakini urafiki walioujenga unaendelea kuimarika.
Baada ya zaidi ya nusu karne, ushirikiano kati ya Tanzania na China umevuka mipaka ya reli na kuenea katika maeneo mbalimbali, yakiwemo bandari, viwanda, kilimo, elimu na mawasiliano ya watu.
Vijana wengi katika vyuo vikuu nchini China pia wameendelea kujifunza Kiswahili, huku mawasiliano na uhusiano kati ya wananchi wa nchi hizi mbili ukiendelea kuimarika siku hadi siku.
Urafiki huu wa zaidi ya nusu karne ni ushahidi kwamba uhusiano wa kweli kati ya mataifa haujengwi kwa maneno pekee, bali kwa mshikamano, kuheshimiana, kusaidiana na kufanya kazi pamoja.
Ni urafiki unaong’ara kama theluji ya Mlima Kilimanjaro na unaendelea kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kati ya watu wa Tanzania na China.


