Na Lucy Ngowi
DODOMA: SERIKALI imeongeza nguvu katika kulinda haki za wabunifu nchini kwa kuweka mifumo itakayowawezesha vijana kusajili, kulinda na kufanya bunifu zao kuwa bidhaa za kibiashara, huku ikisisitiza kuwa ubunifu ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wabunifu hawapotezi fursa kutokana na ukosefu wa ulinzi wa haki miliki na changamoto za kufikisha teknolojia zao sokoni.
Dkt. Nungu ameyasema hayo baada ya kutembelea Banda la Vijana linaloshiriki Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) katika Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samweli Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema COSTECH imekuwa ikijenga mazingira wezeshi kwa wabunifu kupitia utoaji wa fedha za kuanzia, dhamana za mikopo pamoja na kuwaunganisha na taasisi mbalimbali ili kupata mitaji na fursa za kibiashara.
“Serikali haitoi fedha pekee kwa wabunifu, bali inajenga mfumo unaowasaidia kulinda kazi zao, kuziboresha na kuzifikisha sokoni,” amesema.
Amesema katika mazungumzo na wabunifu vijana, wamebaini changamoto mbalimbali ikiwemo usajili wa kampuni, utambulisho wa bidhaa na upatikanaji wa vibali, ambazo zinahitaji kushughulikiwa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Dkt. Nungu amesema moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele ni ulinzi wa haki miliki za wabunifu, akieleza kuwa bunifu isiyolindwa inaweza kupoteza thamani yake na kuwanyima wabunifu manufaa yanayotokana na kazi zao.
Ametolea mfano kijana aliyebuni teknolojia ya kutengeneza mbolea kwa kutumia nywele, ambaye baada ya kupata msaada wa COSTECH katika usajili na ulinzi wa haki zake za ubunifu, aliweza kupata uwekezaji na fedha kutoka nje ya nchi.
“Hii inaonyesha umuhimu wa kuwa na mifumo ya kuwawezesha wabunifu kuanzia hatua ya wazo hadi kufikia soko,” amesema.
Aidha, amesema COSTECH imepokea maombi ya vijana kuhusu changamoto za marejesho ya mikopo inayotolewa na halmashauri, ambapo wameomba muda wa kuanza kulipa uongezwe ili kuwapa nafasi ya kuendeleza miradi yao.
Amesema suala hilo litajadiliwa na mamlaka husika ili kuboresha mazingira ya mikopo kwa vijana wabunifu na wajasiriamali.

