Na Lucy Lyatuu Dodoma
CHAMA Kikuu cha Ushirika Cha Tunduru (TAMCU) kimesema kinajivunia thamani ya chama hicho kuongezeka kutoka Sh bilioni 1.5 hadi zaidi ya Sh bilioni tano kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na kuimarika kwa shughuli za uzalishaji na biashara za ushirika.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha korosho katika wilaya ya Tunduru,jengo la utawala lenye ghorofa tano linaloghagimu sh bilioni saba.
Mjumbe wa Bodi wa chama hicho, Nurdin Chakilo amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya nanenane jijini Dodoma
Amesema mafanikio hayo ni sehemu ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa na chama hicho, ikiwemo uendeshaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala, uuzaji wa pembejeo za ruzuku na ujenzi wa miundombinu ya kuongeza thamani ya mazao.
Amesema mfumo wa stakabadhi umesaidia kurahisisha huduma kwa wakulima, hususan katika upatikanaji wa pembejeo, hatua ambayo imechangia kuongeza tija na uzalishaji wa mazao.

Amesema Chama kilikuwa kimetoka kuwa na thamani ya sh bilioni 1.5, lakini sasa, kutokana na miradi inayotekelezwa na chama ya zaidi ya bilioni tano,” amesema.
Amesema chama hicho pia kinaendesha ghala na shughuli za pembejeo, huku kikiendelea na mipango ya kuwekeza katika miradi mikubwa inayolenga kuongeza thamani ya mazao na mapato ya wanachama.
Ameongeza kuwa chama hicho kina matarajio ya kuongeza zaidi uzalishaji katika msimu unaoendelea, huku kikihimiza wakulima kutumia vizuri fursa za pembejeo na huduma zinazotolewa kupitia ushirika.
Kuhusu ujenzi wa jengo amesema linatarajiwa kuwa na ukumbi mkubwa wenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watu 700, pamoja na maeneo mengine yatakayopangishwa kwa ajili ya kuongeza mapato ya chama.
Amesema hatua za awali za mradi huo tayari zimeanza, zikiwemo taratibu za upatikanaji wa vibali, ramani na maandalizi mengine muhimu kabla ya kuanza ujenzi.
Amewataka vijana nchini kutumia fursa zilizopo katika vyama vya ushirika na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo na uchumi wa nchi.
Amesema ushirika siyo mfumo unaohusu wazee pekee, bali ni sehemu ya uchumi inayohitaji ushiriki wa makundi yote, hususan vijana ambao wana nafasi kubwa ya kuleta mawazo na ubunifu mpya.
Ametoa wito kwa wananchi na wadau wanaotembelea Maonesho ya Nane Nane kufika katika banda la chama hicho ili kujifunza kuhusu huduma, miradi na fursa mbalimbali zinazotolewa na ushirika.

