Na Lucy Lyatuu,Dodoma
TAASISI Ya Utafiti Ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imebainisha kuwa mfumo wa kidigitali unaotumia teknolojia ya satelite wa vua,uza na nunua (PFZ) unasaidia wavuvi kutambua maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na samaki.
Tayari mfumo huo umesajili wavuvi zaidi ya 1000 nchini na unawasaidia wavuvi kupata maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na samaki, ambapo wananchi zaidi ya 3,000 wamekuwa wakiulizia taarifa za maeneo ya kuvua kupitia mfumo huo
Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dkt. Ismael Kimirei, amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kwenye maonesho ya kilimo Nanenane.


Dkt. Kimirei, mvuvi anaweza kutuma ujumbe kwa simu akieleza eneo alipo na anapopanga kwenda kuvua, ambapo mfumo hutumia taarifa hizo na kutoa mapendekezo ya maeneo yenye samaki wengi.
“Baada ya kuvua, mvuvi hutuma picha ya samaki alionasa na taarifa hizo kupitia mfumo huo, jambo linalomwezesha mnunuzi kumtafuta moja kwa moja bila kupitia kwa madalali,”amesema.
Dkt. Kimirei amesema mfumo huo pia unasaidia wavuvi kupata fursa ya kukopesheka kutokana na taarifa za shughuli zao za kifedha zinazohifadhiwa ndani ya mfumo.
Amesema TAFIRI pia imeanza kutumia teknolojia ya kupima ubora wa maji kwenye mabwawa ya ufugaji wa samaki ili kuwasaidia wafugaji kubaini mapema mazingira yanayoweza kuhatarisha uzalishaji.

“Teknolojia hiyo kwa sasa imeanza kutumika mkoani Mwanza kwa kushirikiana na vikundi vya vijana wa BBT pamoja na baadhi ya wananchi, huku lengo likiwa kuwafikia wafugaji wengi zaidi nchini”,amesema.
Amefafanua kuwa vifaa hivyo vinaweza kutoa taarifa za mapema kuhusu mabadiliko ya mazingira ya maji, ikiwemo uchafuzi wa maji, upungufu wa oksijeni na kushuka kwa joto la maji, hali zinazoweza kuhatarisha maisha ya samaki.
Dkt Kimerei amesema teknolojia hiyo inamwezesha mfugaji kujua mapema kama mazingira ya maji hayako salama kwa samaki vilevile mfugaji kuchukua hatua haraka za kuvuna samaki au kutafuta suluhisho kabla ya kupata hasara.
Amewataka wavuvi na wadau wa sekta ya uvuvi kutembelea banda la TAFIRI katika maonesho ya Nanenane kupata elimu zaidi na kuendelea kujisajili na kutumia teknolojia hizo ili kupunguza gharama za kwenda kuvua bila uhakika wa kupata mavuno.

