Na Lucy Lyatuu, Dodoma
WAZIRI Mkuu ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Kwamba uwekezaji wake umeendelea kuongeza uzalishaji wa mazao,kuimarisha usalama wa chakula na kuinua kipato cha wananchi.
Ameipongeza benki hiyo kwa mchango wake katika kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini, huku akiitaka kuongeza uwezo wa kifedha ili kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuharakisha mageuzi ya uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara.
Mwigulu amesema hayo baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma.

Amesema Serikali inahitaji kuona TADB ikijengewa uwezo mkubwa zaidi wa kifedha ili iwe chanzo cha uhakika cha mitaji kwa sekta ya kilimo, akibainisha kuwa utegemezi wa ruzuku pekee hauwezi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakulima nchini.
Ameitaka TADB kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TAMISEMI kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao ili kuboresha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, hatua itakayowawezesha wakulima kuhifadhi mazao yao, kuyatumia kama dhamana ya mikopo na kuuza wakati bei zinapokuwa nzuri.
“Maboresho hayo yataongeza tija katika biashara ya mazao, kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna na kuongeza thamani ya uzalishaji wa wakulima,” amesema.
Akizungumza, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi ya kimkakati inayobadilisha sekta ya kilimo nchini, ikiwemo umwagiliaji, mazao ya biashara na miradi ya kuongeza thamani ya mazao.

Amesema zaidi ya sh bilioni 700 zimetolewa kufadhili miradi ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini, huku vyama vya ushirika vinavyozalisha kahawa, hususan katika mikoa ya Kagera na Kigoma, vikiwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo.
Nyabundege amesema TADB pia imewezesha mradi wa kisasa wa uzalishaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo, unaotumia teknolojia ya kisasa iliyopatikana kutoka Misri, ambayo kwa sasa ina uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi kwa kuzingatia viwango vya utunzaji wa mazingira.
Amesema mradi huo umefungua soko kubwa la samaki, umeongeza thamani ya mazao ya uvuvi na umeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kwanza katika ukanda kutumia teknolojia hiyo ya kisasa katika sekta ya uvuvi.
“Tunaendelea kufanya vizuri katika kufadhili miradi yenye tija kwa uchumi wa nchi. Lengo letu ni kuhakikisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi zinakuwa nguzo kuu za maendeleo ya uchumi,” amesema Nyabundege.

