Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAKALA wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) umewataka wafugaji nchini kuchanja mifugo dhidi ya ugonjwa wa homa ya kutupa mimba, ukielezwa kuwa ni tishio kubwa kwa uzalishaji wa mifugo, uchumi wa wafugaji na afya ya binadamu.
Daktari Mtafiti wa Magonjwa ya Mifugo kutoka TVLA, Issack Mengele, amesema ugonjwa huo umeenea katika mifumo mbalimbali ya ufugaji, lakini umeonekana kwa kiwango kikubwa zaidi kwa ng’ombe wanaofugwa kwa mfumo wa malisho huria unaotumiwa na jamii nyingi za wafugaji na wakulima.
Amesema tafiti zinaonyesha maambukizi ni madogo kwa ng’ombe wanaofugwa ndani, lakini yanaongezeka kwa kiasi kikubwa katika mifumo ya ufugaji wa asili kutokana na mwingiliano wa mifugo na ukosefu wa hatua za kinga.
Mengele amesema hatari ya ugonjwa huo inaongezeka zaidi kwa binadamu, hususan katika jamii zinazotumia maziwa mabichi bila kuyachemsha, jambo linalochangia maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa wanyama kwenda kwa watu.
Amefafanua kuwa wagonjwa wengi hupata homa ya muda mrefu ambayo mara nyingi huchanganywa na malaria au homa ya matumbo, hivyo kushindwa kupata matibabu sahihi kwa wakati.
“Ugonjwa huu unaweza kusababisha mtu kupoteza nguvu za kufanya kazi na wakati mwingine kupoteza maisha endapo hautatambuliwa mapema,” amesema.
Kwa upande wa mifugo, amesema ugonjwa huo husababisha ng’ombe kuharibikiwa na mimba, kupungua kwa uzalishaji wa maziwa na kuathiri uzazi, hali inayosababisha hasara kubwa kwa wafugaji na kudhoofisha ukuaji wa mifugo.
Amesema katika baadhi ya maeneo nchini kiwango cha maambukizi kinafikia kati ya asilimia 15 hadi 20, huku maeneo machache yakiripoti viwango vya hadi asilimia 30 au 40, ingawa bado hakuna takwimu za kitaifa kutokana na tafiti kufanyika katika nyakati na maeneo tofauti.
Mengele amesema Serikali kupitia TVLA imeanza kuzalisha chanjo ya Brucellosis kwa ajili ya ng’ombe, akieleza kuwa chanjo hiyo inapendekezwa kutolewa kwa ndama wa kike kabla hawajaanza kuzaliana ili kuwakinga dhidi ya maambukizi.
Amewataka wafugaji kutumia chanjo hiyo kama njia bora ya kuzuia ugonjwa badala ya kusubiri madhara yake, akisisitiza kuwa kinga ni nafuu kuliko hasara inayotokana na kupungua kwa uzalishaji na vifo vya mifugo.

