Na Lucy Lyatuu,Dodoma
BODI Ya Usimamimazi Wa Stakabadhi Za Ghala (WRRB ) ina mpango wa kuanza kuingiza sekta ya mifugo kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni hatua mpya ya kihistoria ambayo inalenga kutoa suluhu kwa wafugaji nchini.
Kwa miaka 20 iliyopita mfumo huu umekuwa ukitumika zaidi kwenye mazao ya kilimo kama mahindi, pamba na korosho.

Kwa sasa WRRB imeamua kupanua wigo wake ili wafugaji waweze kunufaika na mikopo nafuu na masoko ya uhakika kupitia dhamana ya bidhaa zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu, amesema hayo wakati akizungumzia utekelezaji wa miradinya maendeleo kwa mwaka wa fwdha 2025/26 na mwelekeo wa fedha 2026/27.
Kuhusu mkakati wa Bodi kwa miaka mitano ijayo kuanzia 2027 hadi 2031 inapanua wivo wa mfumo wa bidhaa lakini pia kuanza kuinhiza sekta ya mifugo.
Amesema uamuzi huu umetokana na mahitaji makubwa kutoka kwa wafugaji katika mikoa ya kanda ya kati, kaskazini na kusini mwa nchi.

“Wafugaji wengi wamekuwa wakilazimika kuuza mifugo yao kwa bei ndogo wakati wa kiangazi kutokana na ukosefu wa malisho na mtaji. Kwa kuingiza ngozi ghafi, nyama iliyohifadhiwa, maziwa yaliyosindikwa na malisho ya mifugo kwenye mfumo, wafugaji sasa wataweza kuhifadhi bidhaa zao na kupata mkopo wa hadi asilimia 70 ya thamani yake,” amesema.
Amesema kama sehemu ya kuanzisha mfumo huo, WRRB inashirikiana na wizara ya mifugo na uvuvi pamoja na benki za kibiashara kuweka viwango vya ubora na maghala maalum ya kuhifadhia bidhaa za mifugo.
Maghala hayo yatakuwa na vyumba vya baridi, maeneo ya kukausha ngozi, na hifadhi za malisho. Mfugaji akileta bidhaa zake atapewa stakabadhi ya kielektroniki ambayo anaweza kuitumia kupata mkopo au kuuza katika soko la bidhaa.
“Faida kubwa ya mpango huu ni kuondoa adha ya wafugaji kuuza kwa hasara. Kwa sasa msimu wa ukame ukifika bei ya ng’ombe na mbuzi hushuka kwa zaidi ya asilimia 50. Lakini kwa mfumo mpya, mfugaji anaweza kusubiri hadi bei ipande sokoni bila kuogopa kuharibika kwa bidhaa yake. Aidha, benki zitapata uhakika zaidi wa kutoa mikopo kwa sababu stakabadhi itakuwa dhamana rasmi iliyosajiliwa na serikali,” amesema.
Amesema kwa ujumla, kuingizwa kwa sekta ya mifugo kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ni mwanzo wa enzi mpya ya mageuzi katika kilimo cha mifugo nchini.

“Serikali kupitia WRRB inaamini kwamba hatua hii itaongeza mchango wa sekta ya mifugo kwenye Pato la Taifa, kuboresha maisha ya wafugaji, na kuifanya Tanzania kuwa na mfumo imara wa chakula na malighafi kwa viwanda. WRRB sasa inatamka wazi: hakuna tena mfugaji atakayelazimika kuuza kwa bei ya hasara,”amesema.
Kuhusu mikakati mipya ya WRRB kwa mwaka wa fedha 2026/27 amesema inalenga kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuufanya kuwa mhimili mkuu wa uhakika wa masoko na upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo na wakubwa.

