Na Lucy Lyatuu
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetambulisha rasmi mfumo mpya wa kufunga nyaya kwenye nyumba ambao utawezesha kufuatilia matumizi ya nyumba ya umeme kupitia simu ya mkononi mfumo ujulikanao kama smart house.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange amesema hayo wakati akizungumzia mambo muhimu aliyomueleza Rais Wa Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi alipotembeleza banda hilo lililopo katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa maarufu kama Sabasaba.

Amesema kupitia mfumo huo, simu itakuonyesha chombo gani ndani ya nyumba kinatumia umeme zaidi kwa hiyo unaweza ukakizima huko huko uliko.
“Hata kama uko Mwanza, Dubai nyumba iko kigoma unaweza uka switch off hicho kifaa ili matumizi yale unayoyahofia yakasimama,” amesema Twange na kuongeza kuwa ubunifu huo umetokana na Shirika kupata malalamiko kadhaa kutoka kwa wateja kwamba matumizi sio makubwa lakini umeme kuisha haraka.
Amesema malalamiko mengine ni mita kutokusoma vizuri na kuwataka TANESCO kwenda kufanya ukaguzi na mambo mengine,hivyo mfumo huo utatoa suluhu ya kujua chombo kinachotumia umeme mwingi ndani ya nyumba.
Amesema hiyo ni teknolojia mpya ambapo wataizindua muda si mrefu kuisambaza kwa wateja jamno linaloonesha kuwa wahandisi wameumiza vichwa na ni jambo hilo liko mezani.

Amewataka wateja wa umeme kuendelea kujua kwamba kila siku wanaumiza vichwa kadri wanavyopata changamoto kutoka kwao na wanaumiza vichwa vya kutafuta suluhu ya changamoto zao.
Hata hivyo alimshukuru sana Rais zanzibar Dkt Mwinyi kupata muda wa kutembelea banda la tanesco na kuona mambo mengi wanayoyfanya.
Amesema amemweleza Rais Dkt Mwinyi hatua zinazochukuliwa na Shirika juu ya kutekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia na kwamba wameshapewa maelekezo ambapo wanatengeneza mbinu tofauti tofauti za kutekeleza
” kwa hiyo kwa sasa tuna mpango unaitwa ni bill financing ambao unaendelea hapo wateja wetu ambao ni wapya na wale ambao tayari wanatumia umeme wanaweza wakakopeshwa majiko na wakawa wanalipa mkopo wao kadri wanavyonunua umeme,” amesema.
Amesema mpango umekuwa na mwitikio mzuri wa mafanikio zaidi ya asilimia 90 kwa hiyo umefanikiwa na ndio maana wameingia kwa sekta binafsi ambao wako nao kama wadau.
“Tumesaini nao mikataba na tumeanza kazi ya kukopesha majiko haya kwa wananchi kwa hiyo naendelea kutoa wito kwa wananchi wote wasiogope kutumia umeme tayari wenzao wameshaonyesha njia hii ndio nishati nafuu zaidi kuliko nishati zingine,” amesema na kuongeza kuwa wanasayansi na wahandisi wameshatengeneza majiko ambayo yanatumia umeme rafiki na utafurahi ukilinganisha na gharama unazitumia kutumia nishati nishati nyingine.

Aidha amesema amemueleza Rais Dkt Mwinyi kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.
Amesema katika mradi huo utakuwa na njia za umeme tatu za kupita chini ya maji ikiwa inatoka Dar es Salaam kwenda Unguja kutoka Tanga kwenda Pemba na ya kwenda Mafia.
Amesema ule ni mradi mhandisi mshauri atapatikana Agosti na wanatarajia kumpata mkandarasi Januari na muda wa utekelezaji ni miezi 20, 22.
Twamge amesema mradi kukamilika kwake utaongeza uwezo wa kupeleka umeme mwingi zaidi zanzibar ambayo imejengwa sana katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Dkt Mwinyi.

