Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Mafinga Mjini, Dickson Lutevele, ameihoji serikali kuhusu kuchelewa kwa malipo ya madai ya wafanyakazi wa zamani wa Kiwanda cha Karatasi cha SPM Mgololo, akisema wamekaa muda mrefu wakisubiri haki yao bila mafanikio.
Akiuliza swali la msingi bungeni jijini Dodoma, Lutevele ametaka kufahamu ni lini serikali itatekeleza malipo hayo, akibainisha kuwa kuchelewa huko kumeendelea kuwaathiri wahusika kiuchumi na kijamii.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo amesema wafanyakazi hao walishinda kesi mwaka 2007 ambapo mahakama iliamuru walipwe na pande zote mbili serikali na mwekezaji lakini hadi sasa hawajalipwa.
Amehoji pia kama serikali haioni umuhimu wa kumaliza mgogoro huo kwa wakati ili kurejesha haki ya wafanyakazi hao.
Lutevele amerejea kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuacha tabasamu kwa Watanzania, akisisitiza kuwa wafanyakazi hao wanastahili kulipwa fidia yao haraka baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema madai hayo yanatokana na mchakato wa ubinafsishaji wa kiwanda hicho mwaka 2004 uliosababisha baadhi ya wafanyakazi kupunguzwa kazi.
Ameeleza kuwa mwekezaji tayari amelipa sehemu ya madai yanayomhusu, huku serikali ikibeba jukumu la upande wake kama mmiliki wa awali kabla ya ubinafsishaji.
Londo ameongeza kuwa serikali ilitenga fedha kwa ajili ya madai hayo mwaka wa fedha 2017/2018, lakini baadhi ya wadai walikataa kupokea wakidai kiwango kilichotolewa hakikutosheleza.
Hata hivyo, amesema serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kumaliza mgogoro huo, huku akibainisha kuwa suala hilo bado liko katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi.

