Na Lucy Ngowi
ARUSHA: WAANDISHI wa habari wameaswa kuandika habari zinazohamasisha amani na kuzingatia usalama wao wanapoandika masuala ya migogoro.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Waandishi wa Habari ya Kusaidia Jamii za PembezonI (MAIPAC), Mussa Juma, wakati wa mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi unaochochea amani na namna ya kujilinda wanapotekeleza majukumu yao
Juma ameonya kuwa uandishi wa upande mmoja usiozingatia maadili na maslahi mapana ya umma unaweza kuchochea migogoro katika jamii.

Amesisitiza umuhimu wa kufanya uchambuzi wa kina wa habari kabla na baada ya kuchapishwa au kurushwa hewani.
“Tujiulize habari ina madhara au faida gani kwa jamii. Tusiwe na upendeleo, na tuzingatie tahadhari za kiusalama, ikiwemo usalama wa kidijitali na binafsi,” amesema.

Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea John Sendodo amewataka wanahabari kuzingatia sheria za vyombo vya habari hata kama zina upungufu.
Ametaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015 na Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni.
Sendodo, ambaye pia anashirikiana na shirika la kimataifa la Protection Africa, amefafanua vifungu mbalimbali vya sheria hizo pamoja na mikataba ya kimataifa inayohusu taaluma ya habari, akisisitiza wanahabari kutekeleza wajibu wao bila kuvunja sheria.

Mmiliki wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Fanikiwa kilichopo Arusha, Joseph Mayagilla, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.
Amesema uandishi usiozingatia misingi ya kitaaluma umeleta madhara katika jamii.
Mayagilla amependekeza kurejeshwa kwa madawati maalumu katika vyombo vya habari, ikiwemo ya uchunguzi, amani na maendeleo pamoja na uchumi, ili yaongozwe na waandishi wabobezi na kuboresha ubora wa habari.
Naye mtaalamu wa saikolojia, Ester Cornelio, amewataka wanahabari wanaokabiliwa na msongo wa mawazo kutafuta ushauri wa kitaalamu badala ya kujifungia au kutumia pombe na sigara kupunguza maumivu ya kihisia.
Amesema wanaume wengi wamekuwa wahanga wa sonona kwa kushindwa kueleza hisia zao, tofauti na wanawake ambao mara nyingi huzungumza na kupata nafuu.

Wakichangia mada, Meneja wa Dawati la Kidigitali wa Star TV, Tausi Mbowe, na Anthony Mayunga wa Serengeti Media wamesisitiza umuhimu wa maadili ya uandishi, uelewa wa sheria na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo.
Mbowe amependekeza kuwepo kwa mafunzo endelevu kwa wanahabari, hususan kuhusu sheria na usalama wa kidijitali.
Wanahabari wengine walioshiriki, akiwemo Elizabeth Nyivambe (Mbeya), Muta Robet (Geita) na Zakaria Mtigandi (Manyara), wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza mafunzo, hasa katika matumizi sahihi ya mitandao na masuala ya usalama.
Mafunzo hayo yamehusisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Mara, Manyara, Mbeya na Arusha, na yalidhaminiwa na shirika la wanahabari la Press Unlimited.

