Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka Watanzania, sekta binafsi na wadau wote kushirikiana na Serikali katika kulinda na kutunza miundombinu ya uchukuzi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu mafanikio ya Sekta ya Uchukuzi ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, Kipindi cha Pili chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Profesa Mbarawa amesema mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali kujenga miundombinu ya kisasa, salama na yenye tija kwa maendeleo endelevu.

Amesema katika kipindi hicho, Serikali imepiga hatua kubwa katika kufufua Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ikiwemo kukamilisha majadiliano na kusaini mkataba wa uboreshaji wake Septemba 29, 2025 kati ya Tanzania, Zambia na Kampuni ya China ya Ujenzi wa Uhandisi wa Kiraia (CCECC).
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza Juni mwaka huu 2026 na utaongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, biashara ya kikanda na ajira.
Kwa upande wa reli, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa reli za kisasa Dar es Salaam na Dodoma, kuimarisha uendeshaji wa reli ya kisasa ya SGR na reli ya zamani ya MGR, kuongeza vitendea kazi vya usafirishaji wa mizigo, pamoja na kuendelea na ujenzi wa reli ya SGR awamu ya kwanza na ya pili.
Aidha, Shirika la Reli (TRC) limeanza kujitegemea kifedha na kuanzisha kampuni tanzu ya Kampuni ya Reli Tanzania (TANRAIL) kuongeza mapato.
Katika sekta ya bandari na usafiri majini, Serikali inaendelea na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, maandalizi ya Bandari ya Bagamoyo, ujenzi wa bandari na meli katika Maziwa Makuu pamoja na kuboresha usalama wa majini kupitia vituo vya uokoaji na boti za kisasa.
Serikali pia imeendelea kuboresha viwanja vya ndege, kupanua huduma za ATCL na kuimarisha uunganishaji wa kikanda na kimataifa, hatua inayoiweka Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji Afrika Mashariki na Kati.

