Na Lucy Ngowi
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kujenga ushirikiano thabiti na endelevu kati ya taasisi za elimu na sekta za uzalishaji, kwa lengo la kuzalisha rasilimali watu wenye ujuzi, tija na ubunifu ili kuchochea maendeleo ya uchumi jumuishi.
Profesa Mkenda ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, muhula wa pili.
Amesema miongoni mwa hatua zilizotekelezwa ni kuandaa na kutekeleza mpango wa pamoja kati ya Waajiri, Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), vyuo vya kati na vyuo vikuu, unaolenga kulinganisha mafunzo yanayotolewa na mahitaji ya sekta za kipaumbele ikiwemo nishati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na viwanda vya kuongeza thamani.
Ameeleza kuwa mpango huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi na umejengwa katika mfumo wa kiunzi, ambacho kitazinduliwa rasmi Februari 9, 2026 jijini Dar es Salaam.
Kupitia kiunzi hicho, wanafunzi wa VETA na vyuo vikuu watapata fursa ya kupata mafunzo kwa vitendo viwandani, hatua itakayosaidia kuziba pengo kati ya nadharia ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Profesa Mkenda amesema kiunzi hicho kimeoanishwa na sera na mikakati ya kitaifa ikiwemo Dira ya Taifa 2050.
Ameongeza kuwa kupitia miradi ya Mradi wa Kuboresha Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na Mradi wa Kukuza Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kikanda (EASTRIP), pamoja na ushirikiano na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Amali (NACTVET), tayari zimeanzishwa kamati za ushauri wa viwanda na mikataba ya ushirikiano kati ya vyuo na viwanda katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, ujenzi, utalii, madini, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) pamoja na huduma za biashara
Akizungumzia mafanikio mengine ndani ya siku 100, amesema Serikali imeongeza mikopo ya elimu ya juu na kati kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa wanafunzi zaidi ya 276,000, sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Samia Scholarship uliowanufaisha zaidi ya wanafunzi 3,000 katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
Aidha, ameongeza kuwa ujenzi wa shule maalum za sayansi kwa wasichana na shule za vipaji unaendelea, huku kampasi za vyuo vikuu zikijengwa na kukamilishwa katika mikoa mbalimbali nchini, hatua inayopanua fursa za elimu na mafunzo ya ujuzi kwa vijana.

