Na Lucy Ngowi
Dodoma: MBUNGE wa Bagamoyo, Subira Mgalu, amesema Hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imegusa kwa kina miradi ya kimkakati, hususan katika sekta ya viwanda na uwekezaji kwa manufaa ya Jimbo la Bagamoyo.
Mgalu ameyasema hayo wakati akichangia Hotuba ya Rais Samia katika uzinduzi wa Bunge la 13, kuelekea siku 100 za utekelezaji wa Awamu ya Sita, Kipindi cha Pili.

Amesema nia ya Rais Samia ni kuanzisha kongani nyingine ya viwanda katika Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, mradi ambao ulianza kupimwa takribani miaka 15 iliyopita na wananchi wamesubiri kwa muda mrefu utekelezaji wake.
“Kwa mara ya kwanza, Desemba 30, 2025, Wilaya ya Bagamoyo ilimpokea Waziri wa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, akiwa na wawekezaji sita, ambao walikabidhiwa hati ili ndani ya mwaka mmoja wajenge viwanda,” amesema.
Ameongeza kuwa ndani ya siku 100 za utekelezaji, tayari kuna ushahidi wa kuanza kwa ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo baada ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa ujenzi wa gati tatu.
Mgalu amesema miradi hiyo mikubwa imepelekwa katika Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo na kuomba wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya miradi hiyo walipwe fidia stahiki kwa wakati.
Ameeleza kuwa, licha ya kusubiri kwa muda mrefu, Serikali imeanza hatua za kusikiliza na kushirikisha wananchi wa maeneo ya Kondo, Mlingotini, Pande, Zinga, Tiseza na Kiromo.
“Kwa sasa, kutokana na dalili tulizoziona za miradi hii kuanza na maelekezo ya Serikali katika hatua za awali, tuna imani wananchi watalipwa fidia na kupewa makazi mbadala,” amesema.
Akizungumzia mustakabali wa Bagamoyo, Mgalu amesema kuwa kufuatia utekelezaji wa miradi mikubwa, ujenzi wa barabara ya Makofia–Mlandizi pamoja na kipande cha reli ya SGR kutoka Kwala hadi eneo la viwanda, ana imani kuwa ndani ya miaka mitano ijayo Bagamoyo itakuwa mji tofauti kabisa kimaendeleo.

