Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingilia kati changamoto zilizokuwepo katika wilaya hiyo, hali iliyosababisha mambo kuanza kutulia na kuleta matumaini mapya kwa wananchi.
Amesema wananchi wa Ngorongoro wana imani kubwa na Rais Samia na wanaamini uongozi wake utaendelea kuleta mabadiliko chanya na maendeleo makubwa zaidi.
Ndoinyo ameyasema hayo wakati akichangia hotuba ya Rais Samia katika uzinduzi wa Bunge la 13, kuelekea siku 100 za utekelezaji wa Awamu ya Sita, Kipindi cha Pili.

Ameeleza kuwa Wilaya ya Ngorongoro ni eneo la uhifadhi, utalii na ufugaji, ambapo shughuli hizo ndizo vyanzo vikuu vya mapato kwa wananchi.
Hata hivyo, kwa muda mrefu kumekuwepo na sintofahamu pamoja na minong’ono kati ya mamlaka za uhifadhi na wananchi kuhusu matumizi ya maeneo ya hifadhi.
Amesema wilaya hiyo ni kitovu cha uzalishaji kupitia ufugaji na utalii, na kwamba lengo la Rais Samia ni kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni nane ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Amesema ili kufanikisha azma hiyo, alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu, hususan barabara, kwani nyingi bado hazina lami.
Kwa mujibu wake, uboreshaji wa barabara utawezesha watalii kufika kirahisi katika vivutio vyote vilivyopo ndani ya wilaya hiyo, jambo litakaloongeza idadi ya watalii zaidi ya lengo lililowekwa.
Kwa sasa, watalii wengi hushindwa kufika katika maeneo nyeti kutokana na changamoto ya miundombinu mibovu, hususan maeneo ya Loliondo na Serengeti.
Ndoinyo aliongeza kuwa Rais Samia aliwahi kuahidi kutengeneza barabara hizo, na tayari dalili za utekelezaji wa ahadi hiyo zinaonekana kwa kuanza kwa kazi za ujenzi.
Kuhusu sekta ya ufugaji, amesema kuwa jamii ya wafugaji inataka kuona sekta hiyo ikiboreshwa ili iweze kuongeza tija na kuchangia zaidi katika pato la Taifa.
Aidha, alitoa pongezi kwa Rais Samia kwa kuchagua viongozi wasikivu, akieleza kuwa ana orodha ya Mawaziri sita ambao wameonesha nia ya kufika jimboni Ngorongoro kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Alitoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya pamoja na watendaji wa kata kuhakikisha wanachangamka na kufanya kazi kwa kasi ili kuendana na ari ya utendaji ya Rais Samia, kwa lengo la kufanikisha malengo ya maendeleo yaliyojiwekea taifa.

