Na Lucy Ngowi
MBUNGE wa Kisarawe (CCM), Seleman Jafo, amehoji mpango wa Serikali wa kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mzenga–Kisarawe yenye urefu wa kilometa 70 kwa kiwango cha lami.
Jafo amesema barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi wa Kisarawe kwani itachochea ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani.
Aliuliza swali hilo bungeni kwa Wizara ya Ujenzi wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, alisema Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Kasekenya alisema Serikali imeshatambua umuhimu wa barabara hiyo na itaendelea kuitengea fedha kadri zitakavyopatikana hadi ujenzi wake ukamilike kwa kiwango cha lami.
“Tutaendelea kuongeza fedha kadri zitakavyopatikana ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kutokana na umuhimu wake,” alisema Kasekenya.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Kibaha Vijijini (CCM), Hamoud Jumaa, alitaka kujua mpango wa Serikali kuhusu ujenzi wa barabara ya Chalinze–Gwata–Magindu–Mpalu– Utete–Rufiji–Tumbi–Boko–Sofa na Korogwe–Sofa.
Akijibu swali hilo, Kasekenya alisema taratibu za manunuzi zinaendelea ili kumpata mshauri atakayefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya ya Chalinze hadi Utete yenye urefu wa kilometa 354.9 kupitia Bwawa la Julius Nyerere (NHPP).
Aliongeza kuwa usanifu huo unajumuisha kipande cha barabara ya Chalinze hadi Magindu chenye urefu wa kilometa 22.61.
Baada ya kazi za usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo.

