Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewaagiza viongozi wa kisiasa na wa serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kujiunga na kupata uhakika wa huduma za matibabu.
Dkt. Nchemba ametoa agizo hilo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilolo, Dkt. Rita Kabati, wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.
Katika swali lake, Dkt. Kabati alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kutoa elimu ya Bima ya Afya kwa Wote hadi ngazi ya vijiji ili kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na huduma za afya.
Amehoji kuwa, licha ya Serikali kufanya kazi kubwa ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, bado uelewa wa matumizi ya Bima ya Afya ni mdogo kwa wananchi wa vijijini, hivyo kuhoji mikakati ya Serikali katika kutoa elimu hiyo.
Akijibu swali hilo, Dkt. Nchemba amesema Bima ya Afya kwa Wote ni hitaji la muda mrefu kwa wananchi, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kupanua wigo wake tangu mwanzo wa uongozi wake kwa kuagiza taratibu zote za kisheria zikamilishwe.
“Ni kweli hatua iliyobaki kwa kiasi kikubwa ni kutoa elimu kwa wananchi. Bima ya Afya ni msingi wa kuwezesha Watanzania wote kumudu gharama za matibabu, hususan kwa wale wenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya na wasioweza kumudu gharama hizo,” amesema Dkt. Nchemba.
Ameongeza kuwa jambo muhimu kwa wananchi ni kujiunga na mifumo ya bima itakayoelekezwa na Wizara, huku Serikali ikiendelea kufanya jitihada kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa urahisi, kwa uhakika na kwa kuokoa maisha.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kuajiri wataalamu wa afya 5,000 ndani ya siku 100, ahadi ambayo tayari imetekelezwa, ambapo wataalamu hao wamepelekwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali kote nchini.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha majengo ya huduma za afya yaliyojengwa yanakuwa na wataalamu wa kutosha ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Vilevile, Dkt. Nchemba amesema jitihada hizo zinaenda sambamba na upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa katika hospitali mbalimbali nchini.
“Zamani vifaa kama CT Scan na MRI vilipatikana Dar es Salaam pekee, lakini kwa sasa vinapatikana katika hospitali za mikoa, hospitali za rufaa na hospitali za kanda,” amesema.

