Na Mwandishi Wetu
DODOMA: CHAMA cha Wafanyakazi wa Kukusanya Kodi (TAREWU) Taifa kimefanya uchaguzi wake mkuu na kuwapata viongozi watakaokiongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Uchaguzi huo umefanyika jijini Dodoma na kushirikisha wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kabla na baada ya uchaguzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Tumaini Kichila, aliwasisitiza wanachama kushirikiana kwa karibu na viongozi watakaochaguliwa ili kukijenga chama na kukifanya kiwe imara.
Alisisitiza umuhimu wa uongozi kufanya kazi kwa ueledi na kutumia busara pamoja na ushawishi wanapowasilisha hoja za wanachama kwa waajiri, ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.
Uchaguzi ulianza saa saba mchana na kuhitimishwa majira ya saa tano na nusu usiku kwa kutangazwa kwa matokeo.
Akitangaza matokeo hayo, Kichila alimtangaza Lutufyo Mtafya kuwa Mwenyekiti wa Taifa, Fatuma Ramadhan Mshui kuwa Makamu Mwenyekiti, Michael Marere kuwa Katibu Mkuu na Joel Lema kuwa Mweka Hazina.
Aidha, Jennifer Mathias alitangazwa kuwa Mwenyekiti wa Wanawake Taifa, huku Dorothy Raphael Msofu akitangazwa kuwa Katibu wa Wanawake Taifa.
Baada ya kutangazwa mshindi, Mwenyekiti wa Taifa, Mtafya aliahidi kuongoza kwa kuzingatia katiba ya chama.
Aliwashukuru wanachama kwa kumuamini na kuahidi kushirikiana na wagombea wenzake kwa kutumia mawazo yao ili kuendelea kukijenga na kukiimarisha chama.

