Na Danson Kaijage
DODOMA: MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, amesema mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana 2025, ulikuwa mgumu .
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kikatiba cha Jumuiya ya Wazazi kilichofanyika katika Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.
Maganya amesema Jumuiya ya Wazazi ilifanya kazi kubwa kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo, akisisitiza kuwa hatamvumilia mtu yeyote atakayebeza juhudi za jumuiya hiyo.
Ameeleza kuwa wanachama wengi wa Jumuiya ya Wazazi walifanikiwa kushinda nafasi mbalimbali zikiwemo ubunge wa majimbo, viti maalumu, udiwani pamoja na uenyekiti wa halmashauri.
“Nimekuwa mkali kwa wale waliobeza juhudi za jumuiya na nitaendelea kuwa mkali, kwani tulifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kuhakikisha CCM inashinda dola kwa kishindo,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Happi, amesema jumuiya imezalisha idadi kubwa ya wabunge na madiwani.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa, Dogo Idd Mbarouk, amewakumbusha wanachama kuwa katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu, akihimiza ushirikiano na kuepuka makundi.
Wakati huo huo, Baraza Kuu la Umoja wa Wazazi wa CCM limetoa tamko la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Hassan Mwinyi, kwa uongozi wao.
Baraza pia limewapongeza viongozi wengine wa juu wa serikali na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yao.


