Na Lucy Lyatuu
KAMISHNA wa Mamlaka Ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuf Mwenda anawasihi walipa kodi nchini kuendelea kulipa kwa hiari kwa kuwa michango yao husaidia jamii kupata mahitaji yao hususan makundi maalum.
Mwenda amesema hayo wakati akikabidhi shehena ya zawadi za Krismas na Mwaka Mpya kwa Kituo cha Udiakonia cha Kulea Watoto Wenye Ulemavu wa akili cha Mtoni, Temeke na kwa Makao ya Kulea Watoto Yatima Hisani yaliyopo Kibada Kigamboni, Dar es Salaam.

Zawadi zilizotolewa kwa makundi hayo ni pamoja na sukari, mafuta, sabuni, unga, chumvi, vifaa mbalimbali vya usafi, vifaa vya watoto, vyakula na hata fedha .
Akizungumza katika Kituo cha Udiakonia Mtoni, Mwenda amewapongeza viongozi wa kituo hicho kinachosimamiwa na Kanisa La Kiinjili La Kiluther Tanzania (KKKT) kwa malezi yanayotolewa kwa watoto hao kwani yana mchangokubwa

kwao.
Amesema walipa kodi wamekuwa na mchango mkubwa kwa watanzania ambapo hutumika pia kusaidia makundi maalum kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.
Mwenda amewaomba kuendelea kulipa kodi ambayo pia hutumika kuendeleza jamii kwa njia moja hadi myingine.
Kwa upande wake Mratibu wa Kituo hicho Winifrida Malumbo amesema kituo hicho kinasimamiwa na KKKT pamoja na serikali na lengo kubwa ni kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.
Amesema kituo kina watoto 107 wakifundishwa program mbalimbali ili kuweza kujitegemea wenyewe na mzazi huweza kujifunza stad mbalimbali za malezi.
Amesema pia watoto hao hufundishwa elimu maalum, wakipata huduma ya upimaji ili kubaini aina ya changamoto zinazowakabili pamoja na huduma ya matendo mema kwa wenye uhitaji.
Mchungaji wa Usharika wa Mtoni Salome Mwaisenge ameshukuru TRA kwa msaada huo katika kusherehekea sikukuu hizo.

Katika Makao Ya Watotoyajulikanayo kama Hisani, Mwenda amesema kazi ya malezi ni ya jamii yote na kuwashukuru walipa kodi na kwamba kutoa zawadi kama hizo mi ishara ya kutambua mchango wao.
“Kipindi hiki ni cha kushukuru walipa kodi wote Tanzania kwa kuwa mchango wao unatumika pia kusaidia jamii, ” Amesema na kusisitiza uongozi wa Makao kusimamia watoto kusoma kwa bidii.
Amesema yuko tayari kuwa balozi wa kuwasemea watoto wanaomaliza masomo wakitoka katika kituo hicho ili waweze kupata kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Makao hayo Hidaya Mwakitalema amesema watoto wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa usafiri kwa ajili ya kupeleka watoto hospitalini pindi ikitokea tatizo na hata kukosa bima ya afya kwa watoto hao.

