Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KAIMU Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) – Taaluma, Profesa Baraka Maisel, amesema lugha ya Kichina ni zaidi ya chombo cha mawasiliano, bali ni ufunguo wa kufungua fursa pana za kimataifa.
Profesa Maisel ameyasema hayo wakati wa hafla ya utoaji wa udhamini kwa wanafunzi wa Taasisi ya Confucius UDSM kwa mwaka 2025.

Amesema kuwa kadri ushirikiano kati ya Tanzania na China unavyozidi kuimarika katika nyanja mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu, teknolojia ya kilimo, ubadilishanaji wa kitamaduni, utalii na uwekezaji wa kibiashara, ndivyo mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa lugha ya Kichina na uelewa wa mazingira ya nchi hizo mbili yanavyoongezeka.
Ameongeza kuwa Mpango wa Kimataifa wa Udhamini wa Walimu wa Lugha ya Kichina umefanikisha mafunzo ya mamia ya walimu na wataalamu wa lugha hiyo hapa Tanzania, ambao baada ya kuhitimu wamekuwa mabalozi wa urafiki na daraja la ubadilishanaji wa kitamaduni kati ya China na Tanzania.
Akizungumza kuhusu udhamini wa JUYE, Profesa Maisel amesema ni matokeo ya ushirikiano kati ya JUYE Concrete Co., Ltd. na Taasisi ya Confucius UDSM, unaolenga kuwapatia vijana wa Kitanzania fursa ya kujenga mustakabali bora kupitia kujifunza lugha ya Kichina na kuchangia maendeleo ya taifa.
Amewapongeza wanafunzi waliopata udhamini huo kwa kuonesha bidii, uvumilivu na vipaji vya kipekee katika kujifunza lugha ya Kichina, akiwahimiza waendelee kuimarisha ujuzi wao wa lugha, maarifa na maadili, sambamba na kuwahamasisha wanafunzi wengine kujifunza lugha hiyo ili kufungua fursa zaidi za maendeleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius UDSM kwa upande wa Tanzania, Dkt. Mussa Hans, amewapongeza wanafunzi wote waliofanikiwa kupata ufadhili huo kwa mwaka 2025 baada ya ushindani mkali.
Ameishukuru Kampuni ya JUYE Tanzania Ltd. kwa kuunga mkono maendeleo ya elimu kupitia Taasisi ya Confucius.
Dkt. Hans amesema kuwa elimu ni daraja linalovuka mipaka ya kitaifa, hivyo ufadhili huo ni ishara ya kutambua juhudi za wanafunzi waliofanya vizuri na kuwatia moyo kuendelea na hatua zinazofuata za kitaaluma.
Ameongeza kuwa udhamini huo hautawapunguzia tu mzigo wa ada ya masomo, bali utaimarisha uhusiano wa kiutamaduni kati ya China na Tanzania pamoja na kuunga mkono jitihada za Taasisi ya Confucius katika ufundishaji wa lugha na utamaduni wa Kichina.
Amewaambia wanafunzi kuwa kufanikiwa kwao ni matokeo ya jitihada walizozionesha katika kujifunza, licha ya changamoto walizokutana nazo katika kuandika, kuzungumza na kusikiliza lugha ya Kichina.
Amesisitiza kuwa kupitia lugha hiyo, wanafunzi wanapata fursa ya kuifahamu historia na utamaduni wa China uliodumu kwa zaidi ya miaka 5,000 pamoja na kujifunza kutoka kwa taifa linalopiga hatua kubwa za maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JUYE Concrete Co., Ltd., Xu Hongjuan, amesema udhamini huo umeanzishwa kuthamini juhudi za wanafunzi na kutambua umuhimu wa lugha ya Kichina kama daraja la kuunganisha mioyo na kufungua mustakabali wa ushirikiano wa kimataifa.
Amesema kuwa kujifunza lugha ya Kichina kuna changamoto zake, lakini kila hatua ni maendeleo, akiwahimiza wanafunzi kuwa na bidii na uvumilivu. Alinukuu methali isemayo, “Safari ya maili elfu moja huanza kwa hatua moja,” akisisitiza kuwa lugha ya Kichina itakuwa hazina muhimu kwa maisha yao ya baadaye.
Xu Hongjuan ameongeza kuwa JUYE Concrete Co., Ltd. inajihusisha na uzalishaji na usambazaji wa zege pamoja na viungio vya kupunguza maji, na imekuwa ikifanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 kwa kuaminiwa na wateja na kutambuliwa na wahandisi na wasimamizi wa miradi ya ujenzi.





