Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi, amesema tafiti ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kibiashara, akibainisha kuwa bila tafiti hakuna mafanikio ya kweli.
Amesema hayo wakati wa ziara yake katika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) mkoani Dar es Salaam.
Katambi amesema tafiti husaidia kubaini maeneo yaliyokosewa na yaliyofanyika vizuri, pamoja na kufahamu nani alifanya nini na kwa wakati gani, jambo linalosaidia kufanya maboresho na maamuzi sahihi.
Ameeleza kuwa tafiti zinapaswa kuwa dira ya maamuzi ili kujifunza kutokana na makosa ya wengine na kuyaepuka, sambamba na kujifunza kutoka kwa nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Amehimiza umuhimu wa ukusanyaji wa taarifa za masoko ya ndani na nje ya nchi kama jukumu la msingi, pamoja na kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kulinda na kusimamia Muungano.
Aidha, amesema TanTrade ni taasisi muhimu katika kukuza uchumi wa taifa kwa kuongeza mapato, ajira na fursa za kibiashara kwa wafanyabiashara wa ngazi zote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Khamis, amesema taasisi hiyo imefanya tafiti kwa biashara 334, hatua iliyosaidia kuboresha mazingira ya biashara.
Ameongeza kuwa TanTrade imeendesha kliniki za biashara kwa ajili ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara na imeanzisha nembo ya “Made in Tanzania” kwa lengo la kutambulisha na kulinda bidhaa za Tanzania.
Dkt. Khamis amesema hadi sasa bidhaa 30 zimeshasajiliwa chini ya nembo hiyo, na ifikapo Oktoba 2026, makampuni yote yanatakiwa kuanza kuitumia.
Ameeleza pia TanTrade inaendelea kutafuta fursa za biashara, kufanya tafiti za masoko, kutoa taarifa za masoko na bei, pamoja na kujenga uwezo wa wajasiriamali.

