Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHAMA cha COWTU (T) kimesema kuwa viongozi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki na uwajibikaji.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mussa Mwakalinga, ameyasema hayo leo Novemba 25, 2025, wakati akifunga mafunzo kwa watendaji wa chama hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa TUCTA, Makao Makuu.
“Kama viongozi, ni vizuri kutambua kuwa uongozi tuliopewa ni tunu na neema kutoka kwa Mungu. Hivyo, yatupasa kuzingatia majukumu yetu kwa kutenda haki,” amesema.

Mwakalinga ameeleza kuwa majukumu ya COWTU (T) ni kudai kulinda na kutetea haki, maslahi, heshima, hadhi na utu wa wanachama wake.
Amewataka viongozi kuhamasisha wafanyakazi kujiunga na chama hicho, kutoa elimu kwa wanachama, kutoa huduma mbalimbali na kushughulikia migogoro sehemu za kazi.
Aidha, amewataka viongozi kuhakikisha matawi ya chama yanakua na kusimamiwa kwa nidhamu, huku wakitumia ipasavyo wasimamizi wa kazi.
Naye Katibu wa chama hicho Kanda ya Mashariki, Seka Kitori, amesema vyama vya wafanyakazi vinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ushirikiano.

“Tunapotembea kwa pamoja, tuhakikishe tunatembea kwa pamoja kwa uhalisia. Ni vizuri idara ya kazi ikatekeleza wajibu wake,” amesema.
Kwa upande wake, Subira Mwasamboma kutoka Idara ya Rasilimali Watu amesema kuwa kuna haja ya mabadiliko katika masuala yanayohusu vyama vya wafanyakazi.

Naye Ofisa Elimu Msaidizi, Nancy Mwansasu,amesema kuwa baadhi ya changamoto zilizopo zinahitaji viongozi wenyewe kuanza kubadilika. “Tunahitaji mabadiliko,” amesema.
Mafunzo hayo yalijikita katika mada mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya sheria za kazi na utekelezaji wake, historia ya vyama vya wafanyakazi, kuanzishwa kwake, majukumu yake, uhusiano kati ya vyama, serikali na waajiri, pamoja na mbinu za utatuzi wa migogoro sehemu za kazi.





