Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE mteule wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, amesema kuwa Rais amemleta kiongozi bora atakayetimiza vyema majukumu ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Chitanda amezungumza hayo muda mfupi baada ya Bunge kuthibitisha jina la Waziri Mkuu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan Kulipendekeza.
Amezungumza hayo leo Novemba 13, 2025 katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Amesema tangu kiongozi huyo, Nchemba alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, miradi mingi ya maendeleo nchini imefanikiwa kutokana na usimamizi wake mzuri wa fedha na juhudi za kuongeza mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema kwa msingi huo, miradi ya maendeleo imekuwa ikitekelezwa katika kila wilaya nchini.
Pia Chatanda ameeleza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu kumekuwa na ongezeko kubwa la wanawake waliogombea na kushinda majimbo mbalimbali.
Amesema kampeni za UWT ziliwahamasisha wanawake wengi kugombea, matokeo yake wanawake wamefanikiwa kushinda takriban majimbo 37, huku wengine 114 wakipata nafasi za Viti Maalum.
Amesema wanawake hao wanatarajiwa kuwasilisha bungeni changamoto zinazowakabili wanawake nchini, hususan katika masuala ya kiuchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri inayotakiwa kutolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inatolewa ipasavyo ili kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Chatanda pia amekumbusha ahadi ya Rais Samia ya kutenga Sh. Bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo.
Amesema UWT itahamasisha wanawake wengi kunufaika na mikopo hiyo ndani ya siku 100 za utekelezaji wa mpango huo, kama alivyoelekeza Rais.

