Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Segerea, Agnesta Lambart (CHAUMA), amesema licha ya upinzani kuwa wachache katika Bunge la 13, anaamini kuwa uwakilishi bora hauhitaji wingi wa wabunge, bali hoja zenye tija kwa maendeleo ya wananchi.
Amesema hayo katika viwanja vya Bunge, leo Novemba 11, 2025 Jijini Dodoma.
“Wingi si kigezo cha ubora. Hata tukiwa wachache, tunaenda kuleta tofauti kubwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Lambart.

Akimpongeza Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu amesema ana imani naye kutokana na uzoefu wake kama kiongozi aliyewahi kuwa Naibu Spika, na anaamini Bunge litafanya kazi kwa ushirikiano na serikali katika kuwatumikia wananchi.
Lambart, ambaye amechaguliwa kwa kura zaidi ya 256,000, amesema ushindi wake umetokana na imani ya wananchi waliotambua utendaji wake wakati akiwa mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA, ambapo alijipatia heshima kwa hoja zenye mashiko zilizowasilishwa bungeni.
“Wananchi wa Segerea wananitegemea sana. Wanahitaji maendeleo na wanataka sauti yao isikike bungeni. Nitaendelea kusimamia yale yanayowagusa moja kwa moja,” amesema.
Mbunge huyo amesema licha ya Segerea kukua kwa kasi, bado kuna changamoto nyingi katika miundombinu, maji, afya, elimu na uchumi.
“Segerea imesahaulika kwa muda mrefu. Barabara hazipitiki, maji safi na salama hayapatikani, akina mama bado wanatembea umbali mrefu kuchota maji. Nitahakikisha dhana ya ‘Kumtua mama ndoo kichwani’ inatekelezeka kikamilifu katika jimbo langu,” amesema.
Aidha, amesema atahakikisha wananchi wa kipato cha chini, wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wanapata mikopo isiyo na riba ya asilimia 10 kutoka halmashauri, kama njia ya kuwawezesha kiuchumi.
Akizungumzia elimu, Lambart amesema atapigania kuondoa mzigo wa michango mingi kwa wazazi, kwani sera ya serikali inasema elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita ni bure.
“Nitahakikisha shule zangu zinapata ruzuku ya kutosha ili kuwapunguzia wazazi mzigo wa michango, hasa kwa kuwa wengi ni wa kipato cha chini,” amesema.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa vipaumbele vyake vikuu ni kuboresha miundombinu, maji safi na salama, afya, elimu na uchumi, akiahidi kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha wananchi wa Segerea wananufaika na matunda ya maendeleo.

