Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Kilolo, Rita Kabati (CCM), amesema katika Bunge la 13 anatarajia kufanyika kwa mabadiliko makubwa yatakayowaletea wananchi maendeleo ya kweli.
Amesema hayo nje ya viwanja vya Bunge alipozungumza na Waandishi wa Habari katika Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 13, Dodoma.
Amesema tayari amefanya tathmini ya changamoto zilizopo katika vijiji vyote vya jimbo hilo na amejiandaa kuzitafutia ufumbuzi kupitia vikao vya Bunge na ushirikiano na serikali.
“Nimekuwa mbunge ninayeuliza maswali mengi yenye maslahi kwa wananchi, jambo lililowajengea imani kwamba ninawapigania kwa dhati. Sasa naenda kutekeleza yale yote niliyokuwa nikiyasema bungeni,” meisema Kabati.
Mbunge huyo amebainisha kuwa changamoto kubwa katika jimbo la Kilolo ni barabara zisizopitika wakati wa mvua, hali inayokwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Niliahidi kwa wananchi wangu kuwa nitahakikisha maeneo korofi yanatengenezwa ili barabara ziweze kupitika muda wote. Tayari upembuzi yakinifu umefanyika, hivyo kazi inaanza mara moja,” amesisitiza.
Kabati amesema hatakwenda bungeni kwa maneno matupu bali kwa vitendo, akisisitiza kuwa dhamira yake ni kutumikia wananchi kwa uaminifu na uadilifu.
“Siji kuremba, nakuja kazini. Wananchi wameniamini, nami nitahakikisha sitawaangusha. Tunataka kuwaonyesha Watanzania kuwa wanawake wanaweza, na tunataka idadi ya wabunge wanawake wa majimbo iongezeke kwa sababu tunafanya kazi,” amesema.

