Mwandishi wetu.Babati
HATIMAYE tuzo ya Uhifadhi unaoshirikisha jamii, iliyoshinda mwezi uliopita Taasisi ya Uhifadhi na Utalii ya Chem Chem Safaris, iliyopo eneo la hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge, wilayani Babati Mkoa wa Manyara,imewasili nchini, serikali imepongeza.
Tuzo hiyo, imetolewa na Taasisi ya kimataifa African Travel and Tourism Association(ATTA) ya nchini Uingereza, ambayo ilishirikisha nchi mbali mbali duniani.
Tuzo hiyo baada ya kufikishwa nchini sasa inatarajiwa kufikishwa serikalini na wizara ya Maliasili na Utalii kama.sehemu ya kuunga mkono jitihada kubwa za Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii na Uhifadhi nchini, kufungua milango katika.sekta ya Utalii na uhifadhi, kuhamasisha maelfu ya watalii kuja nchini.
Rais wa ATTA, Nigel Vere Nicoll, ndiye alitangaza ushindi wa tuzo ikiwa ni sehemu ya vipengere vinane ambavyo vinatambulika na shirikisho la Utalii duniani vilivyokuwa vinashindaniwa.
“Baada ya majaji kupitia sifa za kila taasisi na pia kupokea maoni kutoka kwa watalii waliotembelea maeneo hayo, Taasisi ya Chemchem ndio ilikuwa mshindi wa kwanza wa jumla wa tuzo ,hasa baada ya kuweza kushirikisha jamii katika eneo la Burunge WMA katika uhifadhi na Utalii na jamii kunufaika “amesema
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja Mkuu wa Chem Chem, Clever Zulu alishukuru ATTA kwa kuwapa tuzo hiyo na kutambua mchango wa Chem Chem katika Uhifadhi.
Zulu amesema tuzo hiyo sio ya Chem Chem peke yake bali ni tuzo ya Serikali, Tuzo ya Burunge WMA, Tuzo ya Wananchi wote hususani wa wilaya ya Babati mkoa Manyara ambao wamekubali ardhi yao itumike kwa uhifadhi na Utalii na wanashiriki kuitunza.
Ofisa Wanyamapori mkoa Manyara, Felix Mwasenga amepongeza Chem Chem na Burunge WMA kwa ushindi wa tuzo hiyo,
Amesema serikali inatambua jitihada za uhifadhi ambazo zinafanywa na Chem Chem, hivi sasa zinatambuliwa kimataifa.
“Tutaipokea taarifa za tuzo hii na itafikisha kwa viongozi wetu wa mkoa kuonesha jinsi mkoa Manyara unavyofanikiwa katika uhifadhi na Utalii.
“Tumeona ushindi huu na tunauthamini sana kwani utaongeza watalii kuja mkoa Manyara na hivyo kuongeza mapato ya serikali na wananchi”alisema
Kwa upande wake, Meneja wa hotel ya chemchem, Elizabeth Omboi amesema ushindi huo una maana kubwa kwao na utavutia watalii zaidi.