Umoja Wasisitizwa Kama Msingi Wa Mtangamano Wa SADC
Na Mwandishi Wetu
ANTANANARIVO, MADAGASCAR: UMOJA na mshikamano vimeelezwa kuwa silaha kuu ya kuimarisha mtangamano wa kweli ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kufuatia makabidhiano rasmi ya uenyekiti wa Kikao cha Maofisa Waandamizi kutoka Zimbabwe kwenda kwa Madagascar.
Makabidhiano hayo yalifanyika Agosti sita, mwaka huu 2025 jijini Antananarivo, ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Madagascar, Eric Ratsimbazafy, amepokea uenyekiti kutoka kwa Balozi Albert Chimbindi wa Zimbabwe, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa.
Katika hotuba yake ya kuaga, Balozi Chimbindi ameeleza kuwa licha ya changamoto za kimataifa kama UVIKO-19, ukame, na mabadiliko ya tabianchi, SADC imeendelea kuwa imara kiuchumi na kunufaika katika nyanja za ulinzi, usalama, viwanda na huduma za kijamii.
Ametoa wito kwa nchi wanachama kushirikiana zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, nishati na maji ili kuongeza kasi ya maendeleo na ajira kwa vijana, akisema rasilimali watu na maliasili ni nguzo muhimu za ustawi wa kanda.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban.
Kikao hiki ni miongoni mwa vikao vya maandalizi kuelekea Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika Agosti 17, 2025.