Na Mwandishi Wetu
WANACHAMA zaidi ya 800 wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Sekta ya Umma (TUGHE) wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ili kuunga mkono jitihada za kukuza utalii wa ndani na kutambua fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.

Katibu wa TUGHE, Hery Mkunda, amesema ziara hiyo imewasaidia wanachama kupata uelewa mpana kuhusu thamani ya urithi wa asili wa taifa.

Pia Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka TANAPA, Steria Ndaga, amewapongeza kwa kuunga mkono utalii wa ndani, akieleza kuwa shughuli kama hizo huchangia pato la taifa na kutoa ajira kwa vijana.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Jully Bede Lyimo, amesema kwamba utalii wa ndani una mchango mkubwa katika kukuza biashara ndogo ndogo, kuongeza mapato na kuimarisha uzalendo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro, Amri Mtekanga, ametoa maelezo kuhusu vivutio vilivyopo pamoja na taratibu za kupanda mlima huo.
Pia washiriki wamepata fursa ya kushuhudia vivutio mbalimbali vikiwemo maporomoko ya maji, mimea ya kipekee na mandhari ya kuvutia ya Mlima Kilimanjaro, maarufu kama ‘Paa la Afrika’.

Ziara hiyo ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani na inaonesha mshikamano wa Watanzania katika kuendeleza sekta ya utalii nchini.
